USHUHUDA WA MUNA LOVE

Nilipata badiliko la maisha kupitia kwa mtoto wangu wa miaka sita, baadaye alifariki dunia

 “MUNGU anazo njia nyingi anazotumia kuokoa watu wake, kwa ajili ya kusudi lake mwenyewe. Alimtumia mtoto wangu akiwa na umri wa miaka sita, kugeuza mtazamo wangu wa imani, siku chache baadaye Mungu alimtwaa.”

NILIZALIWA Mkoani Lindi mnamo mwaka 1989, natoka katika familia iliyochanganya dini mbili tofauti,  mama akiwa ni Muislamu na baba yangu  Mkristo.

Nilibahatika kusoma mpaka kidato cha pili lakini kutokana na changamoto mbalimbali za kimaisha yaliyoikabili familia yangu, sikuweza kuendelea mbele na masomo  ya elimu ya Sekondari, nikaamua kujiingiza katika maisha ya starhehe nikiwa na umri mdogo.

  • MAISHA YA DUNIANI,YALINIWEKA MBALI NA MUNG

Nilikuwa binti niliyependa starehe za dunia na nilipenda sana ugomvi. Nilijikuta nikipigana  mara kwa mara na  wenzangu. Mwaka 2012 nilipata uja uzito na kujifungua mtoto wa kiume niliyemuita jina la Patrick.

Mwanangu Patrick alichelewa sana kutembea kutokana na hali ya maisha ya dhambi pamoja.  Alipofikisha miaka mitano nikalazimika kumpeleka hospitali kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari, ndipo walipobaini kumbe alikuwa na tatizo la  kulika mifupa ya nyonga.

Nakumbuka kutokana na tatizo hilo daktari alishauri afanyiwe upasuaji. Hivyo alifanyiwa upasuaji ya kwanza, lakini hakupata nafuu yoyote, na wala hakuweza kutembea.

Madaktari wakashauri mwanangu akatwe mguu, kauli iliyonishtua  sana, nikagoma mtoto wangu asikatwe mguu.

  • Safari ya Mungu kusema na nafsi yangu

Nakumbuka wakati madaktari wanajipanga kumfanyia oparesheni ya sita, nilistaajabu kusikia  mwanangu Patrick, akiimba nyimbo za Kikristo kwa mara ya kwanza.  Nikakumbuka wakati mwingine aliponiambia mama; naomba tumuombe Mungu, na siku zingine  aliniomba  nimpeleke kwa Mchungaji akaombewe.

Kumbuka kwamba mimi nilikuwa natoka katika familia zilizochanganya dini mbili, Uislamu na Ukristo, hivyo wakati mwingine nilipuuza mawazo na kauli zake.

Nakumbuka kuna siku moja  aliniomba nimuitie Mchungaji amuombee, siku hiyo niliamua tu nimridhishe asije kunisumbua tena, nilimuita Mchungaji alipoombewa mwanangu akaniambia mama mimi nimepona.

Tukatoka hospitali ya Muhimbili tukarudi Kunduchi lakini kutokana na ule muujiza alionishuhidia mtoto tulipokuwa hospitalini niliamua  moja kwa moja tukafikie kanisani Mikocheni “B’ Assemblies of God, kwa mama Getrude Rwakatare.

Tulipofika kanisani hapo baada ya kuombewa, mwanangu akapokea uponyaji, akatupa magongo, akipiga kelele;  ‘mama nimepona.’ mimi ni mzima.’ Suku iliyofuata nilipompeleka tena hospitali kwa daktari wake, lakini baada ya uchunguzi wa madaktari wakaniambia kuwa mtoto anaendelea vizuri.

Nakumbuka siku moja Patrick akaniambia kuwa, mara kwa mara amekuwa akitokewa na Yesu, na kuondoa  chupa zote za bia zilizopo ndani ya nyumba yetu. Kumbuka maisha ya starehe ya kunywa pombe ndiyo yalikiwa yangu.

Kuna siku pia Patrick, alinilazimisha   kwenda kanisani, japo kwa siku hiyo sikupenda, nakumbuka  tulipofika kanisani tukamkuta mtoto mmoja anaumwa sana.

Chaajabu nilichokiona kwa mtoto Patrick alimuombea yule mtoto mwenziye na baada ya kumuombea yule mtoto alipona palepale huku tukishuhudia.

Vitendo alivyofanya mtoto Patrick vilizidi kunistaajabisha na kunitia shaka, na kumuoa kama siyo mtoto wa kaida kwangu, japo wakati fulani nilipuuzia na kujifanya kusahau.

Nakumbuka kuna siku mwanangu alinimbia maneno mazito kwa kusema; “mama nataka Yesu anichukue nikakae nae mbinguni.” Nilishtuka nikamkemea lakini, tangu hapo akaanza kuomba maombi akimsihi  Yesu wake huyo akakae nae pamoja mbinguni.

Baada ya miaze kadhaa alianza kuugua tena, nikampeleka hospitali, baada ya vipimo vya daktari wakabaini  alikuwa na uvimbe kwenye ubongo wake. Hivyo  wakashauri apelekwe Nairobi afanyiwe upasuaji.  Ptrick aliposikia hayo  akasema; yeye hataki kufanyiwa upasuaji bali anataka kwenda kukaa na Yesu mbinguni. Tulichukua hatua na kumpeleka Nairobi lakini alipofika hospitalini alifariki dunia.

Jambo moja ninalopenda kushuhudia, pamoja na kuondokewa na mtoto wangu Patrick, maneno yake yakaanza kunisumbua moyoni mwangu. Nikakumbuka siku moja aliponiambia kuwa; yeye ataondoka kwenda kuishi na BWANA wake Yesu, lakini alinisihi niokoke na kumtumikia Mungu.

Maneno hayo yalizidi kunisumbua sana moyoni, nilipolala kila nilipokwenda, nikiwa kwenye starehe zangu, siku moja nikalazimika kwenda kanisani na kuokoka.

Kwa sasa namshukuru Mungu mara tu baada ya kubadilika na kuokoka, nikaanza kuishi maisha mapya yenye furaha na amani tele. Mungu akaanza kunibariki kuanzia hapo. Nikaacha maisha ya starehe na  nikamuomba Mungu aniongoze nifanye kitu gani, ndipo aliponiongoza kuanzisha  kampuni inayoitwa kwa jina la mwanangu, The Patrick Foundation. Kampuni hii ni mahususi kwa ajili ya kusaidia watoto wasio na uwezo katika jamii inayotoa msaada kwa watoto hao. Hakika Mungu amefanya badiliko la kweli katika maisha yangu. Nikuombe wewe unayesoma ushuhuda huu, utambue kuwa Mungu alikuumba umtumike, inawezekana amesema na maisha yako kwa namna mbalimbali. Usifanye moyo wako kuwa mgumu. Bado neema ipo inayoweza kubadili mtazamo wa maisha yako. Amina.

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

One Comment

  1. Nahitaji kitabu cha nguvu inayobadilisha.
    Nipo mbeya mjini

Leave a Reply to Samwel mmasa Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *