AMOS HAMIS (Shoga Aliyeokoka)

  • Shoga Aliyeokoka

“Nimewahi kuwa kiongozi wa mashoga hapa nchini. Bila aibu, nilivaa mavazi ya kike, bila aibu, na kujipodoa huku nikijiondoa akili na kubadili mwonekano wangu na sauti nikitafuta kufanana na mwanamke mrembo. Hakika, hali niliyokuwa nayo iliwawia vigumu sana watu waliokutana nami, kwa mara ya kwanza, nikiwa katika mawindo yangu nyakati za usiku, kujua kama nilikuwa mwanamke au mwanamume.”

  • Nilikotoka

Yamkini ukashtushwa na historia fupi maisha niliyoyapitia kabla ya kumjua Mungu. Mimi nilizaliwa mwaka 1986, huko Kigoma, nikiwa mtoto wa nane, katika familia ya Mzee Hamisi na mama Hawa Ramadhani. Wazazi wangu waliniita Athman Hamisi. Hata hivyo, watu walianza kuniita shangazi Asu (kwa kizungu AUNT ASU). Jina hili lilitokana na vitendo viovu nilivyovifanya toka nilipokuwa na umri wa miaka 13 tu. Tabia hii ilinipelekea kutengwa na ndugu zangu wa damu pamoja na jamii iliyonizunguka na, kwa sababu hiyo, sikuweza kupata kiwango chochote cha elimu.

Hali hii ilinilemea pale nilipoanza mazoea na watoto wa kike ilihali nikijiepusha na watoto ‘wenzangu’ wa kiume. Tabia hii iliendelea kukua ndani yangu na, mara, niliizoea hadi nikafikia hatua ya kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na vijana wa kiume. Hapo ndipo niliposhuhudia nikipachikwa majina mengi machafu, likiwemo ‘shoga.’ Jamii iliniadhibu kwa kunitenga.  Hata hivyo, adhabu hii haikufua dafu kwangu kwa kuwa, tangu utotoni, niliamua kuishi hivi. Niliyapenda maisha yale huku nikijiona kuwa mwanadamu wa kawaida. Wakati mmoja, nikiwa katika biashara yangu, walijitokeza wenzangu wachache na, baada ya kunituhumu kuwa nilikuwa muovu, walinitenga! Walinichukulia kuwa sikuzingatia maadili tuliyojiwekea.

Tabia hii iliendelea kukomaa na kunipelekea kuwa maarufu, nikijulikana kama Aunt na / au Shangazi Asu. Kama kiongozi wa mashoga, nilivaa mavazi ya kike, bila aibu, na kujipodoa huku nikajiondoa akili kwa kubadili mwonekano na sauti yangu nikitafuta kufanana na mwanamke mrembo. Hakika, iliwawia vigumu watu waliokutana nami, kwa mara ya kwanza, kutofautisha kati ya sura yangu na mwanamke, hasa nilipokuwa kwenye mawindo yangu nyakati za usiku.

Taratibu, sifa zangu zilianza kuvuma! Kila mzazi aliyeniona alinifukuza akinitaka kutojenga mazoea na familia yake.  Nilijihisi mpweke na, ili kuondokana na changamoto hiyo, nilihamia Mwanza. Huko, niliishi mitaani huku nikiendelea kujiuza kwa mwaka mmoja kabla ya kutimikia Arusha nilikoishi kwa mwaka mmoja pia. Hatimaye niliamua kuhamia hapa Dar es Salaam nikiendelea kujiuza ili, pamoja na mambo mengine, kupata namna ya kujikimu kimaisha.

Nimekuwa katika hali hiyo kwa takribani miaka thelathini. Niliishi kama mwanamke ilihali nikipambana na changamoto mbalimbali nilizokutana nazo. Nilichukiwa na kutengwa. Niliambukizwa magonjwa mbalimbali ya zinaa! Maadui zangu waliongezeka huku wengine wakijaribu kuuondoa uhai wangu, bila mafanikio. Jamii ilininyooshea vidole. Hakuwepo mtu, hata mmoja, aliyekuwa tayari kunielimisha kwa kuchukuliana nami katika udhaifu niliokuwa nao!

  • Maisha yangu Dar, hatari tupu!

Hapa Dar, maisha yangu yalizidi kuwa hatarini. Hii ilitokana na kujihusisha kwangu na uovu uliopitiliza. Nilikuwa nikiishi Magomeni Mapipa, katika chumba kimoja cha kupanga, kilichomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa. Nikichukuliwa na wanaume wa kila aina: wakubwa kwa wadogo; baadhi ya wateja wangu walikuwa na hadhi kutoka serikalini na, hata, sekta binafsi. Niliendela kuuzoea mfumo huu wa maisha na kuuona kuwa wa kawaida sana! Wakati mmoja, nikiwa katika harakati zangu, nilikamatwa na Jeshi la Polisi na kutupwa katika gereza la Segerea, nikihusishwa na vitendo vya ushoga. Huu ulikuwa mwaka 2011. Nilifanikiwa kutoa gerezani baada ya kudhaminiwa na marafiki zangu.

KKKT Waniokoa Mikononi mwa Waislam

Nimewahi kunusurika kuuawa na kundi la vijana wa Kiislam! Siku hiyo nilijipiga moyo konde na kwenda katika msikitini mmoja ili, walau, kuswali nikitafuta kupunguza dhambi. Lakini badala ya kukutana na upendo wa Mungu, kama nilivyotarajia, niliambulia kipigo. Kumbe hawakufurahishwa na mavazi yangu; Walistushwa sana kwa namna nilivyokuwa nimevaa! Walinishambulia kwa vipigo mbalimbali. Kama wasingekuwa waumini wa KKKT, Usharika wa Magomeni, hakika ningeuawa. Hao ndio walioninusuru. Kumbukumbu ya tukio lile ilinipelekea kujitenga na nyumba za ibada nikiamini kuwa walinichukulia kuwa adui na mtu nisiyefaa kushiriki katika ibada zao. Tangu siku ile, niliamua kujiepusha na dini.  Niliamini kuwa jamii nzima, isipokuwa wanaume wale niliojihusisha nao kimapenzi, ilinichukia!

Badiliko lililotokea Maisha Mwangu 

Hata hivyo, mnamo mwaka  2013, nilikutana na taarifa zilizonipelekea kupokea badiliko la tofauti sana katika maisha yangu! Haikuwa rahisi, kwa watu wote walionifahamu, kuamini kuwa ningebadilika hata kurejea katika hali ya kawaida. Kusema kweli, hata mimi sikuwahi kuwaza, wala kuota, kama ningefanikiwa kuondokana na ushoga na kuwa mcha Mungu!

Labda unaweza kujiuliza, ‘ndugu huyu alibadilishwa na nani?’ Ilitokea hivi: siku moja nikiwa Magomeni Mapipa, nilikutana na vijana kutoka katika kanisa la Tanzania Assemblies of God, waliopita mitaani, wakishuhudia nyumba kwa nyumba  na kuhubiri Habari Njema za Yesu. Kwa nasibu, vijana wale walipita katika makazi yangu na kunishuhudia. Nilijaribu kuwakatalia lakini, kwa kadri walivyoonesha upendo wao kwangu, nilikubali kuwasikiliza.  Katika mazungumzo yetu, walinieleza habari za Yesu na jinsi alivyonipenda hata kuutoa uhai wake kwa ajili yangu, katika hali yangu ya dhambi! Baada ya kuwauliza maswali mengi na kujibiwa barabara, niliridhika. Hili ndilo lililonipelekea kubadilika! Nilipatwa na mshangao mkubwa! Sikuwahi kuota, hata siku moja, kuwa ningekutana na Mtu anayenipenda zaidi ya wanaume walionilaghai, wakinilipa pesa nyingi, ili kuniingilia kinyume na maumbile!

Baada ya mazungumzo yale, walinikaribisha kwenye mkutano wa Injili uliokuwa ukiendelea huko kanisani kwao. Niliitikia wito na kuwa miongoni mwa watu waliohudhuria katika mkutano ule. Niliketi na kuusikiliza ujumbe, uliohubiriwa, kwa makini! Neno lile lilinigusa sana huku nikisikia sauti ikiniambia, ‘kuchukua hatua, fanya maamuzi.’ Niliitii sauti ile; sikuufanya moyo wangu kuwa mgumu. Nilipita mbele na kuombewa na, toka wakati ule, badiliko la ajabu lilitokea katika maisha yangu.

Mapokezi Ya Furaha

Hakika, tangu kuzaliwa kwangu, sikuwahi kukutana na mapokezi ya furaha, na yaliyojaa upendo, kama yale niliyoyashuhudia siku ile nilipoingia kanisani, kwa mara ya kwanza. Ninasema hivi kwa sababu mchungaji, akiambatana na jopo la viongozi, alinilaki bila kujali muonekano wangu. Uzoefu ule ulinifanya nijihisi kuwa katika ulimwengu wa tofauti. Hakika shangwe, furaha, vifijo, hoihoi na nderemo  zilitawala. Pia, niliwashuhudia watu mbalimbali wakinikumbatia kwa upendo usiokuwa na unafiki! Hali ile iliendelea kunibadilisha kabisa kimtazamo na kujihisi kuwa wa tofauti. Mashoga, waliposikia kuwa nimeamua kuokoka, walinifuata wakinitaka kuyarudia maisha ya awali! Lakini ninamshukuru Mungu kuwa nimeendelea kulitumia Neno lake, kama nililofundishwa, kupitia madarasa ya kuukulia wokovu, na kufanikiwa kujilinda. Hakika, kwa kuwa mwanafunzi mzuri, niliishinda vita ile.

Amani, Furaha katika Maisha Mapya

Niliendelea na mafundisho ya kuukulia wokovu mpaka pale nilipofikia hatua ya ufahamu ulioniwezesha kujitenga na dhambi. Hapo ndipo nilipoanza kutoa ushuhuda wangu kupitia vyombo vya habari mbalimbali vya habari, hapa nchini. Nilifanya hivi ili kuudhihirishia umma kuwa badiliko la kweli, na lililotokea katika maisha yangu, limo ndani ya Yesu pekee. Nilianza kutumika ndani ya kanisa, kupitia uimbaji, na kufanikiwa kutoa albamu nne za nyimbo: Historia ya Maisha Yangu, Shetani Huna Nafasi Tena Kwangu, Msaada Wangu Utatoka Wapi, na Mungu Yuko Upande Wako.

Kuoa Kwangu

Kuoa kwangu kuliambatana na vikwazo, vilevile, kama nilivyotarajia. Ilinibi kupambana na vipingamizi vingi vilivyonikabili  huku nikimuomba Mungu ili anishindie! Habari njema ni kwamba, ulipofika mwaka  2015, Mungu alinijalia kupata mke wa kufafana nami. Nasema hivi kwa sababu, Astilida Juma, ndiye aliyekubali  na kunyenyekea, huku akichukuliana nami, katika hali niliyokuwa nayo. Kupitia ndoa hii, Mungu ametupatia watoto wawili wa kiume, Ebeneza na Israeli. Mpaka sasa, ndoa yetu ina amani tele. Mungu amenifungulia milango mbalimbali ya kibiashara kama vile kuuza nguo na vitu vingine. Nimefanikiwa kumjengea mama yangu, aliye mjane, nyumba kubwa ya kifahari. Ninamtaja mama kwa kuwa baba alifariki dunia siku nyingi!

Mke Aamua Kusimama Nami

Mke wangu aliniambia, baada ya kuoana, kuwa hakuwahi kuwa na wakati mgumu alioupitia kama siku ile nilipomwambia kuwa Mungu alinionesha kuwa yeye, Astilida Juma, alitakiwa kuwa mke wangu. Jambo lile halikuwa rahisi kwake kwa kuwa, siku nilipookoka, nilionekana kwake kama mwanamke. Aliniambia kuwa, hili ilitokana na namna nilivyokuwa nimevalia na kujipamba.  Mwisho ninapenda kukutia moyo kuwa katika hali yoyote unayoiptia Mungu anaweza kukushindia katika hali zote unazozipitia!

 

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *