JAMES YUSTA

  • NILIPOOKOTWA NA MBWA KWENYE DAMPO

“Niliamua kujiua kwa kujinyonga au, ikibidi, kwa kuingia barabani ili nigongwe na gari. Hata hivyo, jitihada zangu hazikufanikiwa kwa kuwa kila madereva waliponiona walifunga breki. Wengine walinitukana huku baadhi yao wakiishia kunizaba vibao. Nilizunguka, nikitafuta kujiua mchana kutwa, bila mafanikio. Hatimaye, ilipofika jioni, niliamua kurudi nyumbani…”

Kama ningeyaelezea maisha yangu, nikitumia neno moja, ningesema kuwa uwepo wangu, duniani, leo ni wa kimiujiza. Mama aliyenizaa alinitupa jalalani nikiwa mtoto mchanga, niliokotwa na msamaria mwema, nilinusurika kutolewa kafara, nimewahi kutupwa kutoka ndani ya treni huko Morogoro na kuokotwa na wasamaria wema nikiwa nimejeruhiwa vibaya na, ajabu ni kuwa, kila aliyejitolea kunisaidia ili niweze kuondokana na maisha ya mitaani alikufa katika mazingira ya kutatanisha!

Mimi, tofauti na watoto wengine, sikubahatika kumpata mzazi ambaye angenieleza kwa usahihi kuwa nilizaliwa lini na tarehe ngapi! Hata hivyo, ninamshukuru Mungu kuwa nilifanikiwa kupata sehemu ndogo tu ya historia ya maisha yangu, kama nilivyosimuliwa na mama mmoja aliyejulikana kwa jina la YUSTA, aliyeniokoa kutoka katika kinywa cha mbwa aliyekuwa katika hatua za mwisho akitaka kunitafunatafuna!

MASWALI MAGUMU YALIYOSUMBUA MOYO WANGU

Mnamo mwaka 1997, nikiwa darasa la pili katika shule ya msingi ya PLAN INTERNATIONAL huko Arusha, na nilipokuwa nikitimiza umri wa miaka saba tangu kuzaliwa, niliamua kumuuliza mlezi wangu swali ambalo nilitamani kumuuliza muda mrefu uliopita! Wakati huo tulikuwa ndani ya gari aliloliendesha na mama, tukirudi nyumbani NJIRO kutoka kujinunulia mahitaji ya kumbukizi la kuzaliwa kwangu huko UNGA LIMITED. Niliamua kuuliza swali lile nikitaka kujua sababu iliyompelekea mama kuonekana mnyonge, mwenye huzuni na kutokuwa na furaha kila ilipofika siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu.

Baada ya kumuuliza swali lile, mama alishtuka sana. Swali lile lilimnyong’onyeza na kuamua kuliegesha gari pembezoni mwa barabara. Ghafla nilimuona akitoa simu janja na kumuita uncle Mayasa, aliyekuwa msimamizi wa miradi yake, aturudishe tulipokuwa. Hali ile iliniogopesha sana. Nilijipiga moyo konde na kumuuliza tena, “Mama,kwa nini unakuwa hivi?” Pia, hakunijibu na, badala yake, alianza kubadilika sura na kuangua kilio. Kuona vile, nilianza kumbembeleza na kumuomba anisamehe kwa kumuuliza maswali yaliyouumiza mtima wake. Nilihisi kuwa nilimkosea mama na kumpelekea kuwa katika simanzi ile! Mara nilimuona uncle Mayasa akiteremka kutoka kwenye taksi na kutuijia tuliokuwa. Mama alifuta machozi haraka haraka na kuhamia kiti cha nyuma ili kumpa uncle nafasi ya kuliendesha gari lile hadi nyumbani.

Tulipofika nyumbani, nikwenda moja kwa moja katika chumba changu cha kujisomea. Nikiwa mle nilitafakari ili kuona kama, yamkini, maneno yangu yalimpelekea mama kukwazika hata kulia machozi. Hata hivyo, sikuona kama lilikuwepo baya lolote nililolinena. Miezi iliendelea kukatika huku maisha yakiwa mazuri kupita kawaida. Kila tulipofunga shule tulisafiri na mama kwenda katika nchi mbalimbali kwa kuwa alikuwa na marafuki wengi wazungu ikilinganishwa na Waafrika. Pia, nilishangaa kumsikia mama akikimudu vyema Kizungu, Kifaransa na Kibraziri kuliko Kiswahili. Ninakumbuka usiku mmoja wa mwezi August (wa nane), akiwa katika chumba chake maalumu cha mazungumzo, mama aliniita na kusema, “mwanangu, nimekuita leo ili tuyazungumzie mambo yale ambayo umekuwa ukinisumbua nayo kila wakati! Je,upo tayari?” Nilimjibu kuwa nilikuwa tayari.

MAJIBU YENYE HUZUNI,KUMBE MAMA ALIYENIOKOA NAYE ALIOKOTWA?

Kuona hivyo, mama alianza kunieleza kuwa yeye ni mtu asiyewajua wazazi wake wala ndugu yeyote wa damu na, kwa sababu hiyo, anaishi kwa neema na upendo wa Mungu. Aliniambia kuwa alilelewa na kusomeshwa na Bruda mmoja, marehemu Justine Stewart, raia wa Ujerumani, alipokuwa Mmisionari huku Afrika, alisema siku moja, mnamo mwaka 1978, alipokuwa akisoma katika chuo cha Sayansi nchini Italia, yeye na wazazi wake walikuwa wakihamia katika nyumba nyingine na, kwa nasibu, akaokota cheti kilichomhusu yeye. Alipokisoma cheti kile aligundua kuwa wale hawakuwa wazazi wake na, kwamba, alikuwa na asili ya Afrika Mashariki katika mji unaoitwa Tanganyika. Aliniambia kuwa, awali, alijiuliza maswali mengi akitaka kujua kwa nini yeye awe mweusi ilihali mtu aliyemwamini kuwa baba yake awe mzungu, tena, bruda asiyeruhusiwa kuoa wala kuwa na mtoto?” Cheti kile kilieleza namna mama huyu (Yusta) alivyookotwa na Stewart akiwa ametupwa ndani shimo la choo. Mwiso wa maelezo mengo ya mama YUSTA, alihitimisha kwa kuniambia kuwa yeye aliokotwa na kulelewa na watu wasiokuwa wazazi wake, Mzee Justine Stewart.

Wakati wote huu nilimsikiliza mama kwa umakini mkubwa. Nilijawa na huruma na, pana wakati, machozi yalinilengalenga! Nilihisi uchungu mwingi, hasa, nilipouona unyama wa mzazi anayethubutu kumtupa mwanawe, aliyembeba kwa muda wa miezi tisa, chooni ili kumuondolea uhai wake! Aidha, nilivutiwa na ujasiri uliochangamana na ubinadamu uliodhihirika kupitia moyo wa Mzee Justine Stewart, aliyeamua kuokoa maisha ya kiumbe ambaye, baada ya miongo mingi, angekuwa Baraka kwangu! Baada ya kifo chake, ndipo nilipobaini kuwa masimulizi yale yalikusudiwa kuniandaa ili niweze kuupokea ukweli wote kuhusu maisha yangu. Mama aliendelea ambapo, sasa, baada ya kubaini kuwa alikuwa na asili ya Tanganyika, alitafuta fursa ya kuja kutumika katika eneo lililo karibu na alikookotwa na, hii, ilimpelekea kuhamia Nairobi, Kenya. Jambo ambalo, yamkini, hakulijua ni kuwa Mungu alimuongoza ili aweze kuja huku na kuninusuru na mauti ya kabla ya wakati wake, kama ilivyomtokea pia.

Hatimaye mama Yusta aliamua kunielezea kile kilichopelekea huzuni yake kila ilipofika kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa. Katika maelezo yake, nilibaini kuwa, tukio lile lilimkumbusha ukweli kuhusu maisha yake mwenyewe. Hili lilimhuzunisha na kumliza! Alinieleza kuwa, siku moja mnamo saa 10:00 za alfajiri, akiwa katika visiwa vya Lamu, aliondoka katika hoteli aliyofikia na kwenda kumuabudu Mungu, katika kanisa lililokuwa jirani. Lakini alipokuwa akiingia katika uzio wa kanisa lile, alishangaa kuwaona mbwa wanne, waliokuwa pembezoni mwa dampo, wakiliburuza boksi lililoonekana kufungwa kwa kamba za katani. Kuona vile, alirudi hotelini na kuwaomba walinzi wawili waliokuwa zamu ya usiku ili wamsindikize na kujionea kilichokuwa kikiburuzwa na mbwa wale. Mara alipofika karibu na mbwa wale, aliona damu ikichuruzika kutoka ndani ya boksi lile na kuwaomba walinzi wawafukuze mbwa wale. Mbwa walipokimbia, mama aliwaomba walinzi wamsaidie kulifungua lile furushi.

Alinieleza kuwa, kilichomsukuma na kumpelekea kulifungua lile boksi kilitokana na pamba za uzazi alizobahatika kuziona zikining’inia. Hili lilimfanya kuamini kuwa mlikuwemo na mtoto katika boksi lile, alimkuta mtoto, aliyeviringishiwa kwenye furushi la nguo na kuanza akiwa hai. Alilitumia boksi lile lile kumbeba mtoto mpaka kwenye nyumba za masista na kuwaelezea namna alivyofanikiwa kumuokota kichanga kile huku akikiosha na kukipatia huduma zilizohitajika. Walikwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi na kupewa hati iliyowataka kumlea kichanga tajwa mpaka pale mama au baba yake atakapojitokeza. Hivi ndivyo mama huyu alivyokabidhiwa mtoto huyu ili aweze kumhudumia. Mama huyu alifurahi sana kumpata mtoto kwa kuwa aliamini kuwa huyo alikuwa amepewa kama zawadi kutoka kwa Mungu na, kwamba, angekuwa ndugu yake wa damu!

Nilimsikiliza mama kwa umakini mkubwa aliponisimulia mkasa huu! Alisema kuwa, baada ya siku tatu, alirudi jijini Nairobi na kuanza maisha ya huduma huku akiendelea kumlea mwanawe huyo. Ilipofika mwaka 1990, mtoto wake walipokuwa akitimiza umri wa mwaka mmoja, alipata nafasi ya kuhamia Moshi, nchini Tanzania, kikazi. Akiwa huko ndipo alipoamua kujikita katika shughuli za maendeleo na kuanza kutekeleza mipango ya kuachana na utawa. Alifikia uamuzi huo ili kutafuta muda wa kuendelea na huduma zingine zilizougusa moyo wake. Ilipofika mwaka 1995 ombi lake la kutaka kuuacha utawa lilikubaliwa na, ndipo, alipohamia Arusha. Baada ya maelezo haya, mama alitoa albamu na kunionesha picha zangu nikiwa kichanga na nilipookotwa huko Kenya. Pia, alinionesha picha zake, akiwa kichanga, nililia sana baada ya taarifa hiyo.

Mama naye alilia kwa uchungu huku akinibembeleza. Kwa shingo upande nililazimika kuyaamini maelezo niliyopewa kwani sikuwahi kudhani kuwa Yusta hakuwa mama yangu mzazi. Baada ya wiki mbili mama, alipokuwa akitoka Moshi kufuatilia miradi yake, alipata ajali mbaya ya gari na iliyopelekea kifo chake. Siku moja, kabla ya kifo chake, mama aliniita na kunipa hati za nyumba tatu, kadi ya benki, na kadi tatu za magari. Jioni ile mama alitukutanisha mimi na wafanyakazi wake wote. Jambo hili lilinifanya kuwa na wasiwasi kuhusu mambo yalivyokuwa yakijiri. Katika mkusanyiko ule alituasa kuishi kwa kumhofu Mungu.

Uncle Mayasa, aliyekuwa msimamizi mkuu wa miradi ya mama enzi za uhai wake, alinona mimi kuwa kikwazo katika kutekeleza mipango yake. Jambo moja lilikuwa dhahiri na lenye manufaa kwake: mimi kuondolewa uhai. Na hili alidhamiria kulitekeleza kwa ustadi mkubwa.

Siku moja nikiwa shuleni, nilifuatwa na mwanafunzi mwenzangu, Frank, na kuniambia kuwa ninaitwa na uncle Mayasa.Nilipotoka nje ya geti la shule, nililiona gari lililokuwa likitumiwa na uncle likiwa limeegeshwa kando ya mti. Ajabu ni kwamba nilipoingia ndani ya gari sikumkuta uncle. Badala yake gari liliondolewa kwa kasi ya ajabu kuelekea Mererani. Njiani, nilijazwa vitambaa mdomoni, nilifungwa kamba mikononi na miguuni na, niliwasikia wakizungumzia habari za kutolewa kafara, ndipo nilipojua kuwa uhai wangu upo hatarini. Baada ya safari ya muda mrefu, tulifika, nami nilishushwa kwa kubebwa juu juu huku mvua kubwa ya upepo ikiendelea kunyesha. Nililazwa mchangani. Mara alikuja mtu na kunifunga kitambaa kizito usoni. Nilihisi kizunguzungu na giza nene wala sikutambua nilipokuwa kwa kuwa ulikuwa ni usiku mnene. Mara niliona kama mwanga wa tochi ukimulika kuja pale nilipokuwa na, kabla hawajanifikia, kilisikika kishindo kikubwa, ngurumo tatu za radi zilizofuatiwa na vilio na kelele zilisikika. Pale nilipokuwa ardhi ilikuwa ikitikisika. Kwa macho yangu niliwaona wale waliokuwa wameshikilia tochi, wakinijia, wakiwa wameangukiwa na mti na kufukiwa na udongo. Nilipopata ufahamu, nilijikuta nikiwa nimezungukwa na wamasai. Hawa ndiwo walioniokota nikiwa nimetelekezwa na wauaji katikati ya mapori!

  • MAISHA YANGU MITAANI, KUFUNGWA GEREZANI

Nilishihudia maisha yangu yakichukua mkondo mwingine tofauti na nilivyotarajia. Nilinyang’anywa urithi wangu wote niliokuwa nimeachiwa. Hata nilipojaribu kurudi nyumbani, tulipoishi, nilifukuzwa mithili ya mwendawazimu! Mazingira yale yalinipelekea kujiunga na watoto wa mitaani. Huko ndiko kukawa nyumbani petu. Tulilala mabarazani, mitaroni na, wakati mwingine, makaburini! Nilishinda na kulala njaa mara kwa mara. Jamii ilitutenga wakiamini kuwa tulikuwa wezi. Nilishuhudia baadhi ya marafiki zangu wakigongwa gari na kufa papo hapo; wengine wakipigwa na raia kwa kudhaniwa kuwa ni wezi; Nilikamatwa na kuswekwa gerezani Zanzibari kwa kosa la uzururaji, Niliteseka sana na maisha huko gerezani.Ninamshukuru Mungu kuwa, katika haya yote, alinishindia na kutoka!

  • MAISHA YA KUKATA TAMAA, NALITAMANI KUJIUA

Hapo ndipo nilipoamua kujiua, iwe ni kwa kujinyonga, kugongwa na gari, au kwa kunywa sumu. Hata hivyo, jitihada zangu hazikufanikiwa kwa kuwa kila madereva walioniona walisimamisha magari yao. Wengine walinitukana na, baadhi yao walinizaba vibao. Kwa kweli nilizunguka, nikitafuta kutimiza azma hiyo, bila mafanikio. Hatimaye, nilichoka na kurudi nyumbani. Maisha yaliendelea kuwa magumu sana na, kwa sababu hiyo, niliamua kujimaliza kwa namna tofauti kabisa na ile ya kwanza. Awamu hii, nikiwa nimejifungia ndani ya chumba change, nilimeza tembe 24 za klorokwini na kujifunika shuka gubigubi nikisubiri kufa. Ajabu ni kwamba, baada ya saa moja, tumbo lilianza kuuma na ndipo nilipoanza kuharisha mfululizo. Hali ile ilinipelekea kuishiwa nguvu na kuchoka sana. Ilipotimu saa 10:00 za alfajiri nilifanikiwa kupata nguvu kidogo baada ya kunywa maji ya uvuguvugu. Taratibu afya yangu iliimarika. Niliitumia siku ile kukaa nyumbani; sikutoka kwenda kwenye shughuli zangu za kila siku!

Hata hivyo, lile wazo la kujiua lilinirudia tena katika kipindi cha wiki tatu tu. Mara hii, nilinunua pakiti tatu za sumu ya panya na chupa ya maji ya kunywa. Niliyanywa maji yale kidogo na kusaza kama nusu chupa. Nilimimina maji yale katika chupa ile na kuitikisa mpaka ilipobadilika na kuwa nyekundu kama juisi. Ulipowadia usiku, niliinywa sumu ile, mithili ya mtu anayekunywa soda, mpaka ilipoisha. Kwa huruma za Mungu hiyo sumu haikuweza kunidhuru, badala yake niliishia kutapika na kuharisha hadi nilipookolewa na jirani mmoja aliyekuja chumbani kwangu kuazima pasi.

  • NATAMANI KUUZA FIGO, YESU ANAOKOA MAISHA YANGU

Hali yangu iliendelea kuwa mbaya sana kifedha! Hali hii ilinipelekea kushawishika kuuza figo langu ili, walau, nijipatie fedha kwa ajili ya biashara. Siku moja, nikiwa katika harakati za kumtafuta mnunuzi kupitia simu yangu ya mkononi, nilijikuta nikipiga nambari ya mtu mmoja, aliyejitambulisha kwa jina la Joseph, na kuzungumza naye. Tulifikia makubaliano na kupanga namna ya kuonana. Alinielekeza ofissini kwake na hata, siku ilipowadia, tulionana. Cha kushangaza ni kwamba, katika mazungumzo yetu, hakuongelea ununuzi wa figo. Yeye alizungumzia biashara nzuri zaidi iliyonipelekea kumkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yangu (Luke 2:49; 2 Cor. 15:10)!

  • FURAHA NDANI YA BADILIKO LA KWELI

Uamuzi huu ulinifungulia milango mbalimbali katika maisha yangu. Nikiwa katika shughuli zangu za kuosha magari, Mungu alinikutanisha na dada mmoja, Salama, aliyeonekana kuvutiwa na bidii niliyoionesha katika kazi. Dada huyu aliamua kunishika mkono kwa kunilipia pango la nyumba la miaka miwili huko Kinondoni, alinipangishia banda la kufanyia biashara huko Big Brother na kunikabidhi mtaji wa shilingi milioni moja na nusu. Kwa bahati mbaya, Salama alipata  ajali ya gari na kupoteza maisha baada ya kuugua kwa muda mfupi sana! Kifo chake kiliniuma sana. Hata hivyo, wakati huu, tofauti na wakati mwingine wowote, niliamua kumtumaini Mungu (Jer. 29: 11). Niliendelea na shughuli zangu za kuuza nguo na, ingawa biashara ile haikuendelea, kujikuta nikitamani kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu. Siku moja, nikiwa nimeirudia kazi yangu ya kuosha magari, Mungu alinikutanisha na mteja mwingine aliyevutiwa na nyimbo nilizoziimba. Ninaamini kuwa Mungu alikuwa kazini akiniandalia mazingira ya kumtumikia kupitia uimbaji.

Tangu nilipookoka niliendelea kuushuhudia wema wa Mungu katika maisha yangu. Nilikubalika katika makundi mbalimbali ya jamii: wanasiasa, wafanya biashara na, hata, miongoni mwa viongozi wa dini. Nilimuona Mungu akinikutanisha, kwa namna ya ajabu, na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Awamu ya Nne, Mheshimiwa Daktari Jakaya Mrisho Kikwete, aliyezawadia eneo la ardhi huko Kigamboni. Ninatarajia kujenga kituo cha kulelea watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu. Huu utakuwa mchango wangu kwa jamii. Pia, hii itakuwa sehemu ya shukrani zangu kwa Mungu nikikumbuka namna alivyoweza kuniokoa kutoka katika midomo ya mbwa wale waliotaka kunitafuna. Ninaamini kuwa Mungu tunayemwamini, ataniinulia watu watakaokuwa tayari kushirikiana nami katika kuhakikisha kuwa watoto wote wanaozaliwa wanatimiza makusudi waliyoumbwa kuyatekeleza hapa duniani!

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *