Nilipata badiliko la maisha kupitia kwa mtoto wangu wa miaka sita, baadaye alifariki dunia
“MUNGU anazo njia nyingi anazotumia kuokoa watu wake, kwa ajili ya kusudi lake mwenyewe. Alimtumia mtoto wangu akiwa na umri wa miaka sita, kugeuza mtazamo wangu wa imani, siku chache baadaye Mungu alimtwaa.”
NILIZALIWA Mkoani Lindi mnamo mwaka 1989, natoka katika familia iliyochanganya dini mbili tofauti, mama akiwa ni Muislamu na baba yangu Mkristo.
Nilibahatika kusoma mpaka kidato cha pili lakini kutokana na changamoto mbalimbali za kimaisha yaliyoikabili familia yangu, sikuweza kuendelea mbele na masomo ya elimu ya Sekondari, nikaamua kujiingiza katika maisha ya starhehe nikiwa na umri mdogo.
- MAISHA YA DUNIANI,YALINIWEKA MBALI NA MUNG
Nilikuwa binti niliyependa starehe za dunia na nilipenda sana ugomvi. Nilijikuta nikipigana mara kwa mara na wenzangu. Mwaka 2012 nilipata uja uzito na kujifungua mtoto wa kiume niliyemuita jina la Patrick.
Mwanangu Patrick alichelewa sana kutembea kutokana na hali ya maisha ya dhambi pamoja. Alipofikisha miaka mitano nikalazimika kumpeleka hospitali kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari, ndipo walipobaini kumbe alikuwa na tatizo la kulika mifupa ya nyonga.
Nakumbuka kutokana na tatizo hilo daktari alishauri afanyiwe upasuaji. Hivyo alifanyiwa upasuaji ya kwanza, lakini hakupata nafuu yoyote, na wala hakuweza kutembea.
Madaktari wakashauri mwanangu akatwe mguu, kauli iliyonishtua sana, nikagoma mtoto wangu asikatwe mguu.
- Safari ya Mungu kusema na nafsi yangu
Nakumbuka wakati madaktari wanajipanga kumfanyia oparesheni ya sita, nilistaajabu kusikia mwanangu Patrick, akiimba nyimbo za Kikristo kwa mara ya kwanza. Nikakumbuka wakati mwingine aliponiambia mama; naomba tumuombe Mungu, na siku zingine aliniomba nimpeleke kwa Mchungaji akaombewe.
Kumbuka kwamba mimi nilikuwa natoka katika familia zilizochanganya dini mbili, Uislamu na Ukristo, hivyo wakati mwingine nilipuuza mawazo na kauli zake.
Nakumbuka kuna siku moja aliniomba nimuitie Mchungaji amuombee, siku hiyo niliamua tu nimridhishe asije kunisumbua tena, nilimuita Mchungaji alipoombewa mwanangu akaniambia mama mimi nimepona.
Tukatoka hospitali ya Muhimbili tukarudi Kunduchi lakini kutokana na ule muujiza alionishuhidia mtoto tulipokuwa hospitalini niliamua moja kwa moja tukafikie kanisani Mikocheni “B’ Assemblies of God, kwa mama Getrude Rwakatare.
Tulipofika kanisani hapo baada ya kuombewa, mwanangu akapokea uponyaji, akatupa magongo, akipiga kelele; ‘mama nimepona.’ mimi ni mzima.’ Suku iliyofuata nilipompeleka tena hospitali kwa daktari wake, lakini baada ya uchunguzi wa madaktari wakaniambia kuwa mtoto anaendelea vizuri.
Nakumbuka siku moja Patrick akaniambia kuwa, mara kwa mara amekuwa akitokewa na Yesu, na kuondoa chupa zote za bia zilizopo ndani ya nyumba yetu. Kumbuka maisha ya starehe ya kunywa pombe ndiyo yalikiwa yangu.
Kuna siku pia Patrick, alinilazimisha kwenda kanisani, japo kwa siku hiyo sikupenda, nakumbuka tulipofika kanisani tukamkuta mtoto mmoja anaumwa sana.
Chaajabu nilichokiona kwa mtoto Patrick alimuombea yule mtoto mwenziye na baada ya kumuombea yule mtoto alipona palepale huku tukishuhudia.
Vitendo alivyofanya mtoto Patrick vilizidi kunistaajabisha na kunitia shaka, na kumuoa kama siyo mtoto wa kaida kwangu, japo wakati fulani nilipuuzia na kujifanya kusahau.
Nakumbuka kuna siku mwanangu alinimbia maneno mazito kwa kusema; “mama nataka Yesu anichukue nikakae nae mbinguni.” Nilishtuka nikamkemea lakini, tangu hapo akaanza kuomba maombi akimsihi Yesu wake huyo akakae nae pamoja mbinguni.
Baada ya miaze kadhaa alianza kuugua tena, nikampeleka hospitali, baada ya vipimo vya daktari wakabaini alikuwa na uvimbe kwenye ubongo wake. Hivyo wakashauri apelekwe Nairobi afanyiwe upasuaji. Ptrick aliposikia hayo akasema; yeye hataki kufanyiwa upasuaji bali anataka kwenda kukaa na Yesu mbinguni. Tulichukua hatua na kumpeleka Nairobi lakini alipofika hospitalini alifariki dunia.
Jambo moja ninalopenda kushuhudia, pamoja na kuondokewa na mtoto wangu Patrick, maneno yake yakaanza kunisumbua moyoni mwangu. Nikakumbuka siku moja aliponiambia kuwa; yeye ataondoka kwenda kuishi na BWANA wake Yesu, lakini alinisihi niokoke na kumtumikia Mungu.
Maneno hayo yalizidi kunisumbua sana moyoni, nilipolala kila nilipokwenda, nikiwa kwenye starehe zangu, siku moja nikalazimika kwenda kanisani na kuokoka.
Kwa sasa namshukuru Mungu mara tu baada ya kubadilika na kuokoka, nikaanza kuishi maisha mapya yenye furaha na amani tele. Mungu akaanza kunibariki kuanzia hapo. Nikaacha maisha ya starehe na nikamuomba Mungu aniongoze nifanye kitu gani, ndipo aliponiongoza kuanzisha kampuni inayoitwa kwa jina la mwanangu, The Patrick Foundation. Kampuni hii ni mahususi kwa ajili ya kusaidia watoto wasio na uwezo katika jamii inayotoa msaada kwa watoto hao. Hakika Mungu amefanya badiliko la kweli katika maisha yangu. Nikuombe wewe unayesoma ushuhuda huu, utambue kuwa Mungu alikuumba umtumike, inawezekana amesema na maisha yako kwa namna mbalimbali. Usifanye moyo wako kuwa mgumu. Bado neema ipo inayoweza kubadili mtazamo wa maisha yako. Amina.
Nahitaji kitabu cha nguvu inayobadilisha.
Nipo mbeya mjini