USHUHUDA WA BAHATI JOSEPH ONGONG’A

UPONYAJI

“… Niligongwa na lori kubwa la mchanga, lililonichota na kunirusha katikati ya barabara. Walifanya hivi wakiamini kuwa nisingepona! Kutoka pale, nilipelekwa hospitali ya Muhimbili. Walipoulizwa, madaktari, walitahayari wakiamini kuwa sikuwa hai! Nilikatwa mguu wangu wa kulia. Maadui zangu walinicheka. Wengine waliufurahia msiba wangu,wakisema, ’Huyu hatatembea tena. Niliamini kuwa ningepona na kutembea tena! Mungu aliniponya na kunirudishia uzima wangu na, sasa, ninamalizia masomo yangu katika ngazi ya Astashahada ya Ualimu.”

Iilikuwa tarehe 06. 02 2008, nikiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, katika shule moja huko Kigamboni, Dar es Salaam. Ilikuwa jioni, nikiwa na wanafunzi wenzangu, tukirudi majumbani. Ghafla, gari la mchanga (fuso) liliacha njia na kunifuata nilikokuwa. Gari lile, likiwa katika mwendo wa kasi,lilinigonga na kunichota huku likinirushia barabarani! Mashuhuda waliokuwepo hawakuwa na la kufanya; walinifunika kwa nguo! Walionigonga walitokomea kusikojulikana. Waliniacha nikigaagaa. Nilipoteza mapigo ya moyo. Rafiki yangu, tuliyeongozana naye, alilia na kuomboleza! Aliomba msaada, kutoka kwa Wasamaria wema, na kukimbizwa katika hospitali ya Muhimbili. Huko nilikabidhiwa katika idara ya Mapokezi na kutelekezwa kwa zaidi ya saa tatu, bila, walau, huduma ya kwanza. Hayo yakiendelea, wazazi wangu walitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi,’… watoto wenu wamepata ajali; wamepelekwa Muhimbili Hospital, wafuatilieni!

Wakati huo, mama akiwa kwenye ibada ya maombi, alifunga simu ili kuepuka bughudha. Ibada ilipohitimishwa, aliifungua simu yake na kuupokea ujumbe ule. Pia, baba alipokuwa akirejea nyumbani, akiwa Mbagala Rangi Tatu, alipokea simu iliyomtaarifu kuwa nilikuwa nimegongwa. Mpigaji alimtaka kuelekea Muhimbili hospital ili kufuatilia kama nilikuwa hai au la!

Nilitelekezwa Mapokezi

Akiwa amechanganywa na taarifa ile, baba alielekea Muhimbili, kama alivyoelekezwa, na huko Mapokezi alinitafuta, bila mafanikio.  Akionekana kukata tamaa, alipotaka kuelekea mochuari ili, walau, kuubaini kama nilikuwa nimekufa na kujua mwili wangu ulipokuwa umehifadhiwa, akiwa nje ya jengo la MOI huku hajui la kufanya, mlinzi alimshauri kwenda MOI ndani, Idara Inayowahudumia Waliovunjika mifupa. Alipofika huko, aliutambua mkono wangu ulioashiria kuwa nilikaribia kukata roho; macho yangu yaliangalia juu. Baba aliponiona, nikiwa katika hali ile, alipiga kelele na kuwatahadharisha madaktari waliokuwa wakinywa chai katika mgahawa uliokuwa jirani, ”… Kama mtoto huyu, mliyemtelekeza hapa bila kumpa huduma zozote kwa zaidi ya saa tatu, atapoteza uhai wake, basi, mtawajibika.” Hapo ndipo walipoanza kumtuliza na kumhakikishia kuwa ningehudumiwa! Tabia, kama hizi, za kutowajali wagonjwa ndizo zinatafuna nguvu kazi ya taifa. Watu wengi wamepoteza maisha kutokana na uzembe wa madaktari. Serikali inatakiwa kudhibiti tabia kama hizi!

Kutoka hapo, nilikimbizwa mpaka theatre na kutundikiwa chupa tano za maji. Toka wakati huo, nilipoteza fahamu kwa siku tano, mfululizo! Vipimo vilionesha kuwa miguu yangu, pamoja na uti wa mgongo, vilivunjwavunjwa.

Katika kipindi chote hicho, madaktari (wanafunzi) ndiwo walioushughulikia mguu ulioonekana kuumizwa sana. Sikujua sababu iliyowapelekea wataalamu wazoefu kutonihudumia. Kwa uzembe wa wanafunzi hawa, mguu wangu uliishia kukatwa! Hawakuwa makini kwa kuwa waliupuuzia mguu wangu wa kulia,na kuutelekeza kwa siku tatu, huku wakiwa wamekata mishipa yote ya kusafirisha damu,na kuupelekea kuoza. Aidha, wanafunzi wale hawakunihurumia. Hawakuniandaa kisaikolojia, kama ilivyo ada kwa wauguzi! Wakidhani kuwa sikujitambua, waliniambia, kinagaubaga, ”… Huu mguu utakatwa!” Walikuwa katili! Hawakujali kama nilijisikia vibaya au la!

Mama Anihamishia Kibaha

Kauli za madaktari kuwa ningekatwa mguu, zilimuudhi mama na kuamua kunihamishia Kibaha, kwa Daktari Joseph Bake (sasa marehemu). Hakujali vitisho vya madaktari kuwa angeshitakiwa. Tlipofika Kibaha, Bake alishauri kuwa nipewe siku nne zaidi. Taarifa zile zilinistusha sana. Hata hivyo, niliamua kumtegemea Mungu zaidi! Nilijua kuwa, pasipo YEYE, mimi siwezi! Tofauti na kule Muhimbili, Bake alinijali sana kwa kuwa, hata, ilipoamriwa kuwa ningekatwa mguu, aliwaita wazazi na kuwaandaa kisaikolojia ili wao nao, watafute namna ya kunifikishia ujumbe! Wazazi wangu, licha ya kujua kuwa nilitakiwa kukatwa mguu, waliniambia, ”… Tunakurudisha Muhimbili ili ukatengenezewe mguu.”

Jambo lile halikuniteteresha kwa kuwa, tofauti na wagonjwa wengine, Mungu alinijalia kuwa jasiri. Watu walipoona jinsi nilivyowatia moyo, walinishangaa sana. Nilifanya vile bila kujali changamoto iliyonikabili. Wakati wote huo, niliamini kuwa nilikuwa na miguu yangu yote. Ili kunifikishia ujumbe uliokusudiwa, wazazi walimtumia Mchungaji Eliya. Huyu ndiye aliyezungumza nami, kunitia moyo, na kunieleza kuwa mguu wangu, tayari, ulikuwa umekatwa!

Katika mazungumzo yale, Eliya alinisimulia kuhusu majaribu mbalimbali aliyoyapitia Ayubu. Sikujua kuwa alifanya vile ili kuniandaa kisaikolojia. Tukiwa katikati ya mazungumzo yale, alitaka kujua kama ningekuwa tayari kukatwa mguu ule, endapo ingeamriwa. Huku nikijaa imani, nilimhakikishia kuwa nilikuwa tayari, ikibidi, kwa kuwa nilimwamini Mungu! Hapo ndipo aliponiambia, bila kificho, kuwa mguu ule ulikuwa umekatwa tayari! Nilijisikia kama mtu aliyepatwa na kiharusi. Sikuamini kuwa nilichokisikia kilikuwa sahihi! Niliamini kuwa macho na masikio yangu yalinihadaa! Nilimuuliza Mungu,” … Why did this happen?” (Yaani, kwa nini umeruhusu jambo hili litokee?).Hapo ndipo Mungu aliponijibu, “Bahati, jambo hili limetokea kwa kuwa, Mimi, ninakupenda!). Baada ya mazungumzo yale, ilikuja timu ya watu wengine iliyoniombea uponyaji wa haraka!

Hatua ya imani iliyogusa wengi

Niliamua kumuomba Mungu na, ndipo, aliponihakikishia kuwa ananipenda! Niliuguza kwa miezi minane mfululizo, bila kuliona jua. Siku moja, nilichukua hatua ya imani na kutoka nje. Kwa kawaida, mama yangu, kama mzazi, ni jasiri. Yeye, aliniunga mkono na kuniruhusu kutoka nje. Hatimaye, nilifanikiwa kuliona jua! Madaktari walinikimbilia na kunikumbatia, wakinikaribisha duniani, kwa kimombo,”…Bahati, Welcome to the world.”

Mchango Wangu Katika Jamii

Mtu mmoja alisema kuwa Mungu hafanyi jambo bila kusudi. Nami, ninaamini kuwa Mungu amenipitisha katika changamoto hii ili kunipa neema ya kuwatumikia wote wanaopitia mazingira magumu. Ninatarajia kuitumikia jamii kupitia asasi itakayowahudumia watoto (wenye umri mdogo), na makundi ya watu, wanaopitia mazingira magumu. Wengine watakaoguswa na huduma hii ni walemavu na yatima! Taasisi hiyo itatumika kama mwamvuli utakaoyaunganisha makundi mbalimbali ya kijamii yenye uhitaji wa kiroho, kimwili, na, hata, kiakili! Ili kulifanikisha hili, tunatarajia kushirikiana na serikali.

Kwa yeyote unayeniangalia kupitia luninga, mitandao mbalimbali ya kijamii, radio, au unayeusoma ushuhuda huu kupitia magazeti na kitabu ’Nguvu Inayobadilisha’ haijalishi unapitia msukosuko wa aina gani, yupo Mungu anayeinua. YEYE huwafanikisha kwa kuwa, ndani yake, mna nguvu inayobadilisha. Pamoja na yote unayoyapitia, ipo nguvu inayobadilisha. Nguvu hii imenibadilisha. Nimemuona Mungu akiniinulia watu walionisomesha kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita na, hata sasa, wanaendelea kunifadhili katika masomo yangu.

 

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *