JONAS SIMON

NILIPONYWA UKIMWI

“DAKTARI alitumia muda mrefu sana kuzungumza nami na, mwishowe, aliniambia, “kijana enenda zako, wewe ni mzima,jitunze.” Niliishiwa nguvu. Nilianguka chini. Nililia sana. Nilizinduka na kujikuta nikiwa nimezungukwa na kundi la washauri nasaha! Nilipotulia waliniuliza, “kijana una matatizo gani? Bila kusita, niliwaambia kuwa nimekuwa nikiishi na virusi vya UKIMWI kwa miaka minane mfululizo. Kote nilikopima, nilibainika kuwa muathirika.”

Kwa mara ya kwanza, niligundulika kuwa na virusi vya UKIMWI mwaka 2002,baada ya kupima afya yangu katika kituo cha Angaza – jijini Mwanza. Nilifikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa nilikuwa nikiugua homa za mara kwa mara, kukohoa sana, na kuhisi maumivu ya kifua, kwa miezi minne mfululizo.

Daktari alithibitisha kuwa nimeathirika na kunipa kadi namba 21637. Pia,alinishauri namna ya kuenenda ili, walau, niweze kuishi kwa muda mrefu.Licha ya kuonekana kuwa hai, nilijihisi kama mfu. Nililazimika kwenda kanisani na kumtaarifu mchungaji Geofrey Lugwisha wa Tanzania Assemblies of God,tawi la Mwanza, kuhusu msiba ulionikabili.Ushauri wake ulinijenga sana kiimani. Pia, aliomba nami na kunitajia ahadi ya Mungu katika Zaburi 103:3 na kunitaka kulisimamia neno hilo kwa imani.Kwa mara ya kwanza, taarifa zangu, zilichapishwa katika gazeti la Jibu la Maisha, toleo namba 51, na kuthibitishwa na afisa kutoka kituo cha Angaza cha jijini Mwanza, Beatrice Mhando. Lakini, licha ya mtalaamu huyu kukiri kuwa alikuwa na taarifa zangu,hakuwa tayari kuzungumzia hali yangu kwa kuwa, kwa kufanya hivyo, angekiuka maadili ya kazi yake.

Niliendelea kudumu katika kuomba huku nikimwamini Mungu kwa uponyaji.Mnamo mwaka 2003, nilihamia Geita mjini,huku nikiendelea na biashara yangu ya kuuza mitumba. Huko nilijiunga na kanisa la TAG, lililoongozwa na Askofu Simon Masunga, ambaye sikumweleza lolote. Niliendelea kumwamini Mungu huku nikifunga na kuomba.Nilishiriki katika shughuli zote za kanisa na,baada ya miezi kadhaa, nilikwenda katika kituo cha afya cha Geita ili kuhakiki afya yangu tena.Bado vipimo vilithibitisha kuwa niliishi na virusi vya Ukimwi!

Majibu haya yalinyong’onyeza kiimani hata nikajiandaa kufa. Nilimhurumia sana mama yangu mzazi ambaye, kwa wakati huo, aliishi jijini Mwanza. Kwa kweli, mawazo yalinilemea. Maisha hayakuwa na ladha tena! Nilichukua mtaji wa biashara niliyokuwa nikiifanya na kumnunulia mama yangu nyumba ili, kama ikitokea kuwa nimefariki dunia, basi, walau, mwili wangu uhifadhiwe humo. Nilifanya hivi ili kumuepusha mama na kadhia yoyote ambayo ingejitokeza.Pia, nilinunua suti nzuri ya kuzikwa nayo.

Moyoni mwangu, nilijua kuwa ugonjwa huu ulitokana na makosa niliyoyafanya, nilipochochewa na kiburi cha pesa nilizozipata nikiwa kijana. Kila nilipoomba, niliamini kuwa Mungu alinisamehe na,kama ningekufa nikiwa katika hali ile,bila shaka ningeingia mbinguni!Imani hii ilinipelekea kulia mbele za Mungu nikimsihi ili aipokee roho yangu.Maisha yangu yaliyojawa na mashaka sana.Miaka ilienda mbio na, ingawa niliendelea kudhoofu, sikuwa na wasiwasi.

Ndugu yangu alipofariki, mwaka 2008, nililazimika kuusafirisha mwili wake mpaka kijijini kwetu, huko Morogoro.Nikiwa huko nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu, aliyeiishi Dar es Salaam, na kunikaribisha akinitaka nimtembelee ili kutafuta fursa za kibiashara. Nilipofika huko nilijiunga katika kanisa la TAG (Ukonga, Majumba Sita)na kuendelea kuutafuta uso wa Bwana.Siku moja, tulipokuwa tukihitimisha maombi ya kufunga ya siku 21, nililiamini neno la uponyaji lililotolewa na mchungaji na lililowataka wote wenye magonjwa sugu kupita mbele ili waombewe.Baada ya maombi yale, mchungaji aliwataka wote waliomwamini Bwana Yesu kwa uponyaji kupima afya zao na kurudisha majibu siku iliyofuata, yaani Jumatatu.

Kwa upande wangu, sikwenda katika siku iliyopendekezwa na, badala yake, nilikwenda baada ya siku moja kupita. Niliondoka, moja kwa moja,mpaka hospitali ya Amana,Dar es Salaam, na vipimo vilionesha kuwa sikuwa na UKIMWI tena.Awali, daktari alitumia muda mrefu sana kuzungumza nami na, mwishowe,aliniambia, “enenda zako, kijana wewe ni mzima, jitunze.” Ghafla, niliishiwa nguvu na kuanguka chini. Nililia sana. Baada ya kutulia, Madaktari waliniuliza “Kijana, una matatizo gani?” Hapo ndipo nilipowaeleza kuwa nimekuwa muathirika kwa muda wa miaka minane mfululizo. Nilipima katika vituo mbalimbali na kuthibitika kuwa nilikuwa muathirika wa UKIMWI. Aidha,niliwahakikishia kuwa nilikwenda pale ili kuthibitisha uponyaji nilioupokea kwa njia ya maombi.

Daktari alipigwa butwaa. Aliinuka, alinitazama machoni na, kisha, aliniambia, “Enenda zako kijana, Mungu wako amekuponya katika mazingira yasiyoelezeka kisayansi.” Niliondoka na kurejea tena, hospitalini, baada ya miezi mitatu. Kwa mara nyingine, vipimo vilionesha kuwa nilikuwa mzima wa afya tele. Hii ilikuwa mwezi April, 2009! Mwishowe, niliamua kumshirikisha mchungaji na, alipojiridhisha, ndipo aliponiruhusu kushuhudia mbele ya kusanyiko. Ili kujiridhisha, kanisa liliandika barua kwenda katika Hospitali ya Amana,likiomba uthibitisho wa vipimo vyangu na kujibiwa Julai 13 mwaka huo huo. Amana walithibitisha kuwa majibu ya vipimo vilivyosajiliwa kwa namba CODEB 1194,yalimhusu Simon (yaani mimi) na, kwamba,hakuwa mtu huyo (mimi) hakuwa na UKIMWI tena! Muujiza ule uliwashangaza wengi. Mwanasayansi mmoja alikaririwa akisema, “Kimsingi hakuna ushahidi wa mtu aliyewahi kuponywa UKIMWI.Ugonjwa huu hauna tiba.Lakini nimesikia kuwa ipo miujiza. Hili linawezekana kwa Mungu na siyo kisayansi,” alihitimisha.

Maisha Ya Ndoa

Iliniwia vigumu sana kumpata mke wa kuoana naye. Hii ni kwa sababu watu wote, pale mtaani, walinitambua kuwa muathira.Licha ya kushuhudia kuwa niliponywa,kimiujiza, bado nilinyemelewa na roho ya kukata tamaa.Sikuamini kwamba iko siku nitaoa na kuwa na familia, kama ilivyo leo. Hakika Mungu,kwa namna alivyo mwaminifu, aliniwezesha kufunga ndoa na mke wangu,Jacqueline, mnamo Novemba 11, 2011. Tumejaliwa kuwa na watoto watatu: mapacha wawili wa kiume (Daniel na David)na mmoja wa kike(Dorcus). Aidha, Mungu ametupa nyumba huko Mbondole, kata ya Msongola,mtaa wa Majengo Mapya,Ilala.Nimemuona Mungu akitufungulia milango ya baraka katika namna ya ajabu kabisa.

JINSI MUNGU ANIZAWADIA MKE

Siku moja, nikiwa kanisani, katika kipindi cha Uanafunzi na Maandiko, nilikaa jirani na dada mmoja.Wakati somo likiendelea, nilimsikia Roho Mtakatifu akininong’oneza,”…Huyo dada uliyeketi naye, hapo, ndiye atakuwa mkeo.” Ibada ile ilipomalizika, nilimwendea Mchungaji na kumshirikisha hitaji langu na kulipokea vizuri. Hata hivyo, alinitaka kuwa na subira mpaka atakaponiita.

Mwaka ulikatika, bila kuitwa, na, kwa kweli, nilihisi kuwa, yamkini, sikumsikiliza Mungu vizuri.Nililazimika kumfuata Mama Mchungaji,aliyekuwa ameachiwa majukumu yote kwa baba alikuwa safarini. Mama alinishauri niendelee kusuburi lakini sikukubaliana naye! Niliamua kujitafutia mchumba mwingine na kupima afya zetu. Ajabu ni kuwa wazazi wake walikataa tukiwa katika harakati za mwisho za kulipa mahari.

Uchumba ule ulipovunjika, kwa kweli, nililia sana. Mama Mchungaji, aliniliwaza na kushauri kuwa itakuwa vyema kama tutaomba tena.Nilishindwa kuvumilia na, kwa sababu hiyo, nilihamia Zanzibar na kuendelea na biashara zangu huko. Mchungaji aliporudi kutoka Msumbiji, alikokuwa kihuduma, aliniita.Nilipanda Ngalawa, kutoka Zanzibar, na kupitia Bagamoyo.Tukiwa majini, tulinususrika kuzama.Nilitumia masaa matatu nikiupigania uhai wangu.Nilipofika Dar es Salaam, wote watatu (mimi,Mchungaji na Mama),tulimuomba Mungu na kupokea ujumbe kuwa yule binti wa kwanza ndiye alikusudiwa na Mungu kuwa mke wangu.Mama alimpigia simu mhusika, akiwa kijijini kwao – Shinyanga na kuliridhia suala langu.

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *