ASKOFU JOHN SAID MAGENYEKA

 DINI BILA YESU NI MATESO MAKUBWA

Mungu, mimi ni Mwafrika na wewe ndiwe uliyeniumba, Ukristo umenikuta hapa Afrika, hali kadhalika Uislamu, leo hii ukinipeleka Jehanamu kwa sababu ya kutokuwa Muislamu au Mkristo, utakuwa umenionea sana, kwa sababu dini zote hizi zimenikuta hapa Afrika. Nikiwa mimi uliyeniumba naweza kuongea  maneno kama haya, bila shaka na wewe unaweza kuongea, na kunijibu maombi yangu. Nioneshe leo hii njia iliyo sahihi…”

Jina langu naitwa Askofu John Said Magenyeka, ni mzaliwa katika familia ya Kiislamu ya Mzee Said Magenyeka, umri wangu ni miaka 60, naishi Ubungo external, jijini Dar es Salaam. Ni baba mwenye watoto wanne nilioachiwa na marehemu Mke wangu Debora, aliyefariki miaka mitano iliyopita. Tangu utotoni nililelewa katika misingi ya dini ya kiislamu na nilisoma pia elimu ya Msingi na Sekondari.

Nililelewa na kukua katika misingi ya imani hiyo nikielezwa na viongozi wangu wa dini na wazazi  wakinieleza, dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu ni hiyo niliyozaliwa na kulelewa humo na pia nilitahadharishwa kutokuwa na shaka nayo na hata nilielezwa kuwa kiongozi wangu wa dini alikuwa  bora kuliko viongozi wote wa imani zingine duniani. Nikawa na kiburi nikijidai sana.

Nilihitimu Elimu ya Msingi mwaka 1984, na kwa bahati nzuri nilifaulu na kujiunga na elimu ya Sekondari katika shule ya Sekondari Milambo Tabora, mwaka 1985. Wakati huo niliitwa Jafari Saidi. Nakumbuka pale shuleni nilikutana na  mwanafunzi mmoja Mkristo aliyeokoka  aliyejulikana kwa jina la Kiislamu Jafari,  kwakuwa alikuwa ni wajina wangu, akawa rafiki yangu kipenzi na tulishirikiana naye masuala mbalimbali hapo shuleni. Wakati wa chakula tunakwenda wote pamoja, nakumbuka  nilipofika kidato cha tatu, rafiki yangu huyo alinialika kwenda naye kwenye mikutano ya hadhara(injili) ya neno la Mungu, nikawa nampiga chenga.

Siku moja akanialika kwenda kwenye mkutano, akaniambia kuwa, kuna viongozi wanatoka Dar es Salaam, kuja kuhubiri injili hapo Kigoma, twende tukawasikilize. Nikajaribu kukwepa kama kawaida, nikitoa visingizio mbalimbali, nikamwambia  kuwa sijala, akakimbia na kunichukulia chakula, baadaye nikazua kikwazo kingine  kuwa, sijanyosha nguo;  akaninyoshea nguo zangu haraka haraka.

Nilipoona sina kingine cha kujitetea, nikaamua nimtie moyo rafiki yangu, tuliongozana  naye kwenda kwenye mkutano huo, uliokuwa unahubiriwa na Mwinjilisti Moses Kulola, ambaye sasa ni marehemu.

Tulipofika kwenye mkutano huo, rafiki yangu Jafari, akanitafutia kiti cha kukalia,  yeye mwenyewe akaenda sehemu nyingine. Mkutano uliendelea ulipofika wakati wa maombi, niliona mambo ya ajabu sana.

Nilishuhudia watu wakianguka na mapepo wengine wakidondoka na kupona magonjwa yao.  Siku hiyo sikuokoka, japo nilikuwa na shida. Mimi nimetoka kwenye familia inayoteswa na majini na mapepo, hivyo nilipoona majini yanayotutesa na kutuonea yanakemewa na kutoka kirahisi tu, tena kwa maneno, nikawa nashangaa. Baadaye Mhubiri Kulola akasema; kuna kijana yuko hapa anashangaa na kujiuliza maswali mengi, yupo kama mpelelezi hapa, asije akajikuta haya mapepo yanayowatoka watu  yakamuingia yeye na kumpagaa,” Baada ya neno hilo, nikachomoka mbio kutoka kwenye mkutano huo na kurudi shuleni.

Wakati wa likizo uliwadia, nilisafiri kwenda nyumbani, nikiwa na maswali mengi sana kuhusu yale mambo niliyokutana nayo kwenye mkutano huo wa Mzee Kulola. Nilipofika nyumbani nikamsimulia baba yangu kuhusu mambo hayo niliyoyaona kwenye mkutano huo na jinsi mapepo na majini yalivyokuwa yakikemewa na kuwatoka watu kwa jina la Yesu.

Lakini hilo halikumsumbua sana baba yangu, badala yake akaanza kunipa ushuhuda wa mjomba wetu ambaye aliwahi kuombewa na kupona. Baada ya kunisimulia ushuhuda huo, mimi nikamuuliza; baba kama ni hivyo huoni kwamba hawa watu imani yao ndiyo sahihi?

Baba alivyosikia hivyo akanikemea sana akisema; hapana dini yetu ndiyo iliyosahihi,  akaongeza;  Mungu wakati mwingine, anaweza kuwasikiliza makafiri, huku  akinitadhaharisha kuwa, dini nzuri mbele ya mwenyezi Mungu.

Hilo jambo liliacha alama na maswali katika maisha yangu. Baadaye nikaanza kusoma Biblia na vitabu vingine mbalimbali kutafuta ukweli ulipo, nikirejelea masomo ya akina Mazinge, Kawemba na Ngariba, ambao walivuma miaka ya nyuma  kule kigoma  waliohubiri dini ya Usilamu na kutikisa sana. Miaka hiyo Wakristo wengi walisilimishwa sana, nikaanza kufuatilia mafundisho yao ili nipate kujua ukweli na kuitetea dini yangu.

Siku moja nilipohitimu elimu yangu ya kidato cha nne nilipomtembelea rafiki yangu katika kijiji fulani cha Wakimbizi huko Tabora, nikakuta kijiji hicho hakina Msikiti hata moja, nilishangaa sana nikaazimia moyoni mwangu kupanda msikiti katika kijiji hicho.

Nikaanza harakati za kuelezea dini yangu kwa watu, kama ingekuwa wakati huu wanavyofanya Wakristo ningeweza kusema nashuhudia.  Kumbe maneno yangu siku hiyo yaliwaingia moyoni mwa watu wale.  Jioni moja niliporejea kwao, nikakutana nao  wakaniambia kuwa wao walinisikiliza na kwamba, wameamua kufanya maamuzi ya kusilimu na kuwa waislamu. Wakaniuliza niwaelekeze jinsi mtu anaweza kugeuzwa na kuwa Muislamu, wakaniambia kama nitawaelekeza  watakuwa waumini wa kwanza na watakaonisaidia kueneza hiyo imani katika kijiji hicho.

  • Sauti ya ajabu iliyobadili hazma ya moyo wangu na kuacha mshangao mkubwa

Nakumbuka hao watu walikuwa ni Wakristo. Lakini cha kushangaza nilipoanza, kuwaelezea, nikasikia sauti moyoni mwangu ikiniuliza je, wewe mwenyewe unauhakika gani kwamba uko njia sahihi?  Kwa bahati mbaya  bila kutarajia nikayatamka maneno hayo kwa sauti; “Unauhakika gani kwamba uko sahihi? Ghafla nikashtuka na kushangazwa huku nao, wakibaki na mshangao.  Tukatawanyika sote bila kuagana.

Nilipofika nyumbani kaka yake na yule rafikia yangu akaniuliza, kuna kitu kimetokea cha ajabu sana leo, unakumbuka ulipokuwa unawaelekeza  Wakristo waliotaka kuwa Waislamu, ulitamka maneno ya ajabu sana, uliwaambia kuwa wewe mwenyewe huna uhakika na njia yako. Akaniuliza na wewe unataka kugeuka kuwa Mkristo?  Unajua umewaacha watu wameduwaa sana!  Maneno hayo yakazidi kunichanganya sana, na kuniacha na maswali mengi moyoni.  Jioni sikuweza kula kabisa. Nikaanza kuunganisha matukio ya mzee Kulola, matukio mengine kama ushuhuda wa baba, nikaanza kufikiri huenda dini ya Ukristo ni ya kweli, lakini moyoni nikawa najitia moyo kuwa dini ya kweli ni ile niliyozaliwa na kuikuta wazazi wangu wanayo. Nikaanza kuwaza moyoni, nikasema, naweza kuwa Mkristo na nikawa nimepotea au nikawa Muislamu, nikapotea vilevile, lakini nikawaza tena kwa nini Mungu asijitetee mwenyewe?  na kunionesha imani iliyo sahihi!!  Nikaamua kupiga  magoti na kuomba; … Mungu, mimi ni Mwafrika na wewe ndiye uliyeniumba, Ukristo umenikuta hapa Afrika na Uislamu vilevile, leo hii ukinipeleka Jehanamu kwa sababu ya kutokuwa Muislamu au Mkristo utakuwa umenionea sana, kwa sababu dini zote zimenikuta Afrika, nikiwa mimi uliyeniumba naweza kuongea hivi, bila shaka na wewe unaweza kuongea, nioneshe njia sahihi leo. Baadaye nikashtuka, na likaniijia wazo, mbona naomba kama Mkristo? Nikaamua kuondoka na kulala.

  • Nikachukuliwa katika ndoto iliyobadilisha maisha yangu

Ndoto niliyoiota usiku huo, ndio iliyobadilisha kabisa maisha yangu. Niliota niko katikati ya njia mbili zote zinaunganikia kwenye geti moja, kule ndani ya geti niliweza kuchungulia hivi nikaona kuna bustani nzuri na watu wamevaa mavazi meupe, lakini njia zote zinakutana katika geti hilo. Nikaona mtu mmoja akiwa ameshikilia Biblia anakuja na njia ya upande wa kulia, nikajua huyu ni Mkristo, nikawaza moyoni hivi huyu bwana anadhani ataweza kufunguliwa geti hili. Lakini cha ajabu kabla hajafika tu geti lilifunguliwa na akaingia ndani. Baadaye wakati nawaza kuondoka na mimi niingie, nikaona mtu mwingine anatokea kupitia njia ya mkono wa kushoto, nikajua sasa ni zamu yetu sisi kuingia ndani lakini yule mtu alipojaribu kugonga mlango aingie nikimsaidia mlango haukufunguliwa kabisa. Nikashtuka usingizini. Nilipoamka na kutoka usingizini nikaamua moyoni kugeuka na tangia hapo nilianza kusoma Biblia kuliko kitabu kingine chochote.

Tangia siku hiyo, Mungu akanipa kiu ya kusoma Biblia kwa masaa 24.  niliporudi Nyumbani Tabora hakuna aliyejua hilo, nakumbuka ilipofika mwaka 1989 nikaamua kuokoka katika kanisa la Free Pentecostal Church in Tanzania (FPCT).  Tangia siku hiyo wazazi walinifukuza nyumbani na hata nilipooa wazazi hawakutaka kuhudhuria sherehe ya ndoa yangu. Leo nimekuwa baraka sana.  Nina watoto wanne niliowazaa na mke wangu marehemu Debora, aliyefariki miaka mitano iliyopita.  Sasa nachunga Kanisa la Victoria Living Church, lililopo Ubungo external, jijini Dar es Salaam, na nina matawi mengi pia. Baada ya kukutana na NGUVU YA INAYOBADILISHA, Mungu amefanya mambo mengi makubwa katika maisha yangu.

 

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *