MESHAK SALUM HASANI

Nilikumbatia dini na uchawi

“Nilionekana kuipenda dini yangu toka utotoni. Na, hata, nilipopelekwa madrasa, nilijisomea kwa bidii na kufikia darasa la sita la Kiarabu.Toka wakati huo, niliendelea na kufuzu kama ustadhi. Kwangu, mimi, dini ilikuwa kila kitu.”

Mimi nina umri wa miaka 29. Nilizaliwa na kulelewa katika misingi ya dini ya Kiislamu kwa sababu wazazi wangu, wote wawili, ni Waislamu.Katika kukua kwangu, nilijipatia elimu ya madrasa chini ya uangalizi wa waalimu mashuhuri, na kuwa miongoni mwa vijana waliorithi mikoba ya wazee.

Kukabidhiwa Uchawi

Mwalimu wangu, aliyekuwa mganga wa kitabu,alinikabidhi uchawi wa kisomo baada ya kuthibitika kuwa mwaminifu. Tabia ile ilimpelekea mwalimu wangu kuvutiwa nami na kuahidi kunipa zawadi ambayo hakuitaja.Kuanzia wakati huo, alianza kunifundisha namna ya kupiga ramli na,ili kuwa na weledi uliohitajika katika taaluma hiyo, alinipatia fedha za kununulia kitabu cha kutazamia nyota.Kitabu hiki, chenye milango kumi na miwili ya nyota na mashetani, hutoa mwongozo mkubwa sana katika masuala yote ya kichawi.Misingi inayotajwa kuwa ya nyota ni pamoja na Bahethu (Upepo), moto, udongo, na maji.Kupitia elimu hii, niligundua kuwa kuna mashetani wa namna mbalimbali: nge, simba,jua, Mizani inayopishana,nyoka, punda, au sura ya mtu. Maumbo yote haya humfanya mtu kuwa mtumwa.

Umuhimu wa Elimu

Elimu hii,imelenga kuitetea imani ambapo, kwa kutumia ufahamu huu, tuliwashinda maadui zetu. Pia, hutumika kuvuta kinga, utawala, na utajiri. Kwa hiyo, kitabu kinachojumuisha mambo yote haya hujulikana kama ’mjumuiko wa masaa na habari zake au matukio yake katika utawala wa kichawi.’Kitabu hiki kilikuwa na uwezo wa kujieleza, kila saa na matukio yake.Aidha,kilionesha jinsi uganga unavyojali muda kwa kubeba matukio yanayoibukia. Chapisho lile lilijumuisha serikali ya mashetani.Licha ya kuwa mganga wa jadi wa kitabu,nilikuwa mganga wa kienyeji pia. Utalaamu huu niliupata nikiwa darasa la sita, baada ya kuugua na kupelekwa katika pori kubwa ambako nilitelekezwa na kuwaona simba na nyoka wakiwa na vichwa vya binadamu.

Kilichonitokea Kabla ya Kuokoka

Muda mfupi, kabla ya kuokoka, mwaka 2004, nilifika nyumbani kwa ustadhi ili kuwaadibisha wageni kadhaa,akiwemo mama mmoja mlokole.Tulipofika tuliamua kumkejeli! Niliazimia kumkomesha na  usiku utakapowadia, tuliwatumikisha sana. Tuliupata mwanya huu kwa kuwa, miongoni mwao, alikuwepo mganga. Waliosha vyombo usiku kucha, walisafisha nyumba, walilima mashamba na, ilipofika saa 11 alfajiri,niliwarejesha nyumbani, bila kuwaosha. Wale akina mama walipozinduka, kutoka usingizini, walionekana kuwa na vumbi miguuni.Tukio lile lilipelekea mmoja kati yao kuvunja ndoa.

Bado nilipania kumkomoa mama aliyenikaripia akiuliza, ’kwanini mnajadiliana?’Nilitamani kuihamisha nyumba ile na kuifanya ielee juu ya maji! Kwa kufanya hivi,angelala juu ya maji! Kwa hiyo, usiku ule, nilifika alipoishi na kusoma dua ili nyumba ile ipae. Lakini, kila nilipoinyosha fimbo yangu, ili kuifanya nyumba ile kupaa, kulitokea mvutano mkubwa kati ya mkono wangu na nyumba tajwa. Nilipochungulia, kupitia ufa uliokuwa pembeni mwa jengo, sikuona chochote!Nilipoangalia vizuri, niliona moto ukiwaka sakafuni huku ukinikimbiza!Jambo lile lilinishangaza sana!Majini wangu, walipoona kuwa ninazidiwa, walinirusha angani ili kuukwepa moto ule.Nilijitahidi lakini mvuke wa moto ule uliniunguza na kuuguza majeraha kwa majuma mawili,nikiwa kitandani.

Kigoma Yavamiwa kwa Injili

Kwa mara ya kwanza, Domi alikuja Kigoma mwaka 2006,akilenga kuwafikia Waislamu wote katika mji ule. Na, kama ilivyomtokea Herode wakati wa kuzaliwa kwake Yesu Kristo,utawala wa giza katika viunga vyote vya Kigoma, ulitaharuki. Tulilazimika kuitisha kikao ili kubuni namna ya kuwadhibiti makafiri (Wakristo)waliojaribu kuzusha vurugu katika ngome yetu. Kikao kile kilihudhuriwa na zaidi ya mashehe ishirini na, kwa pamoja, tuliazimia kutumia silaha za kichawi ili kuufuta Ukristo. Kwa hiyo, tuliwachagua wawakilishi wanne, miongoni mwetu, na kuwapatia jukumu la kusambaratisha kampeni zilizoendeshwa na makafiri.Majina yaliyopitishwa yaliwajumuisha wazee nguri wa uchawi. Wazee hawa waliahidi kuwa wangetangulia ili kutafiti namna ya kulisambaratisha kundi lile la Wakristo.

Wazee walianza safari yao lakini walipofika huko hawakuliona kanisa na, badala yake, walikuta jiwe kubwa!Jambo lile liliwashangaza sana!Wakati huo huo, niliwafuatilia, kwa mbali na kuwauliza kama wamefanikiwa katika majukumu waliyopewa. Walinijibu kuwa waliwafuatilia lakini hawakufanikiwa. Walinieleza kuwa walifika kwenye chuo cha makafiri lakini hawakufanikiwa kuliona kanisa. Waliamini kuwa lilikuwa limebomolewa! Niliwakatalia na kuwaambia kuwa jengo lile lilikuwepo pale pale pa siku zote.

Mashehe hawakukata tamaa. Walipanga shambulizi lingine lililotekelezwa siku ya tatu. Walifikia kwenye kota za shule iliyomilikiwa na kanisa. Huko nako hawakuliona jengo la shule na, badala yake, waliukuta uwanja mzuri ukiwa umezingirwa na taa kubwa zilizowaka. Niliondoka asubuhi na mapema ili kujiridhisha kama shule ile ilikuwepo na, nilipofika, niliwakuta wanafunzi wakiendelea na masomo.Niliwarudia wazee na kuwauliza, kwa mara nyingine, kama walifanikiwa kuiona shule! Wao waliendelea kunihakikishia kuwa shule ile haikuwepo!

Hata Kabla wiki haijaisha, wazee walirejea na kujieleza, “… Tunashangaa kwa kuwa, tangu tulipoanza uchawi, hatujawahi kuona mauzauza kama haya.” Wakati mmoja walifika katika kanisa la Anglikana na kudai, “… Wakristo wamekuja. Wamefikia kule walikofikia hapo awali.” Walipowafuatilia,waliliona kanisa likiwa limepanda sana hewani. Kila walipojaribu kuroga, hawakufanikiwa!Walishangaa kuiona bahari kubwa iliyoenea katika eneo lile lote huku mtu mmoja, wasiyemfahamu, akicheza danadana juu ya maji.Mashehe hawa walitumia uchawi wao, bila mafanikio. Mimi nilistaajabu sana na, ndipo, nilipoamua kutumia sindano zangu, saba, zilizokuwa na uwezo wa kuua, kila siku, mtu mmoja,kila siku. Hata hivyo, sikufanikiwa! Ilipita miezi miwili tu na wale mashehe (wachawi) wakaanza kufa mmoja mmoja. Mpaka kufikia mwaka 2007, watu sita miongoni mwao walikwisha fariki dunia!

Haukupita muda mrefu, nilibanwa na Mungu katika ndoto na kuambiwa, ‘Hassan, usipoacha uchawi utakufa!’ Sauti ile ilinikosesha amani. Nililazimika kwenda kwenye maombi mlimani, kwa miezi miwili mfululizo,nikimlilia Mungu. Baada ya muda,Mungu alinitahadharisha, ‘Ukitafuta kanisa, litakusaidia.’

Ilikuwa Alhamisi, March 2008, nikiwa pale mlimani, kuanzia saa 4:00 za asubuhi mpaka saa11: 00 za jioni, nilipoongoza na kuingia ndani ya kanisa Katoliki.Nilionana na Padri na kumweleza shida yangu na,ndipo, aliponieleza kuwa mchungaji ndiye aliyejaliwa karama ya kuwaombea wagonjwa na watu wenye matatizo mbalimbali.Nilikubali kuombewa na Mchungaji na, tangu wakati huo, niliamua kuokoka.

Maisha Yangu Kwa Sasa

Ninamshukuru Mungu kuwa, katika wokovu, nilihitimu elimu ya theolojia, ngazi ya stashahada na, mpaka sasa, ninaendelea kumtumikia Bwana kwa kutumia huduma, karama, na vipawa mbalimbali nilivyojaliwa.

 

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *