COSMAS CHIDUMULE

Mwanamuziki Awa Mchungaji

“Siku moja, tukiwa kwenye Onesho la Muziki huko Dodma, mimi na rafiki yangu, marehemu Remi Ongara,nilitokewa na sauti ya ajabu iliyonisumbua sana.Nilijitenga kidogo ili kutafakari. Hata hivyo, nilipothubutu kuingia ukumbini na kujaribu kunywa bia, ghafla, upanga wa ajabu ulionekana ukiwa ndani ya glasi. Niliogopa sana. Nililazimika kuitelekeza pombe ile pale mezani na kukimbilia nje.”

Mimi ni Nani

Mimi nimezaliwa mwaka 1950, katika kijiji cha Mbimbi,Wilaya ya Namtumbo (Ruvuma),mwana wa kwanza wa kiume, katika familia ya Mzee Mdendeule.Licha ya mzee huyu kusomea upadirisho mpaka mwaka 1943, hakufanikiwa na, ndipo, alipoajiriwa na serikali ya Tanzania, kama mpima ardhi.Ninaamini kuwa baba alifuata mkondo wa babu kwa kuwa, huyu, naye, aliitumikia serikali ya Ujerumani enzi za ukoloni.

Baba alihamishiwa Tanga mjini,kikazi,akitokea Ruvuma.Huko nilijiunga na elimu ya msingi mwaka 1958 na,nilihitimu, na kujiunga na ‘Middle School.’Miongoni mwa wanafunzi tuliosoma nao, wakati huo, walikuwa ni pamoja na marehemu Dr. Abdallah Kigoda.Hata hivyo,tuliishi kwa muda wa miaka miwili tu na, baadaye, baba alifariki dunia.Maisha yalituwia magumu sana na kupelekea kukatiza masomo.Pia,kama familia,tulilazimika kurudi kijijini Mbimbi,Ruvuma! Kwa kuwa sikuyazoea maisha ya kijijini,nilihamia Ruvuma mjini na kufikia nyumbani kwa mtu mmoja aliyekuwa rafiki wa karibu wa marehemu baba, enzi za uhai wake, na aliyekuwa kiongozi wa TANU!

Mimi na Muziki

Kwa kuwa kiongozi huyu alimiliki bendi ya muziki, aliniweka kuwa mlinzi na  mtunzaji wa vyombo.Kazi hii ilinipa fursa ya kujifunza namna ya kupiga vyombo, hususani, gitaa.Kipawa changu cha uimbaji kilianza kuonekana siku tulipotembelewa na mgeni mmoja kutoka Kongo, na aliyekuwa miongoni mwa wafanyakazi katika bendi ya mzee.Huyu ndiye alinishawishi akinitaka kuimba naye wimbo aliokuwa ameutunga.Nami,licha ya kuwa na umri mdogo kuliko yeye, nilimwambia kuwa, hata mimi, nilikuwa na wimbo wangu ulioitwa ‘Tanzania ni Nchi Nzuri Sana.Mwanamuziki huyu, alipoyasikia maelezo yangu, alifurahi sana.Huu ndiwo ukawa mwanzo wa safari yangu, kimuziki!

Nilianza kupiga vyombo vya muziki mnamo mwaka 1970,nikiwa na TAS Band huku nikiwa na umri mdogo kuliko waimbaji wenzangu wote.Kupitia band hiyo, nililitetemesha Bass Gitaa, kazi niliyoitekeleza kwa weledi mkubwa na kuajiriwa, moja kwa moja. Kutoka Ruvuma, waimbaji hawa walinitaka tuondoke nao mpaka Dar es Salaam,ili tukatumbuize huko nako! Kwa sababu hiyo, Waliniachia nauli na, siku iliyofuata,nilikutana nao Iringa mjini. Ilikuwa ni mwaka 1971 tuliposafiri nao na kuingia jijini Dar es salaam.Mwaka mmoja, baadaye, ilikuwa dhahiri kuwa nyota yangu iling’ara na ilipofika 1973, nilijiunga na Western Jazz, nilikodumu kwa miaka mine (mpaka mwaka 1977),kabla ya kuanzisha bendi yetu wenyewe,ikiitwa Dar es Salaam international. Bendi hii ilikuwa maarufu sana miongoni mwa vijana wote wa Afrika Mashariki ya wakati ule.

Changamoto ni Fursa

Hata kabla sijaokoka, nilifahamu, fika, kuwa changamoto zaweza kugeuzwa na kuwa fursa! Siku moja vyombo vyetu vya muziki viliungua, tukiwa katika harakati zetu za mwisho za maandalizi ya kutumbuiza.Fundi, alipoona vile,alishauri tukaazime vyombo vingine.Sikukubaliana naye na, isivyotarajiwa,mwaka ule ule,nilianzisha bendi nyingine.Kwa hiyo, changamoto ile ilinipelekea kupigia hatua  nyingine kimaisha.Bendi hii ndiyo ile iliyotoka Mlimani Orchestra, mwaka 1984, na kuitwa DDC Mlimani Park. Aidha,mwaka 1991,Remi Ongala aliniita na kunikabidhi vyombo nilivyovitumia kuanzishia bendi iliyoitwa Serengeti, iliyovunjwa, baadaye mwaka huo huo, na kuundwa kwa Super Matimila Orchestra,kundi lililoniimarisha zaidi kimuziki.

Swali Gumu Laniwewesesha

Siku moja,mimi na wenzangu (akiwemo marehemu Remmy Ongala), tulikuwa kwenye tamasha la muziki huko Morogoro na,lilipomalizika,tulielekea Dodoma.Tukiwa safarini, nilipitiwa usingizi na kusikia sauti ikiniuliza, ”…Cosmas,urafiki wako na Remy Ongala utakapoisha,mwisho wako utakuwa upi? Kwa kweli, nilishtuka sana na kutoka usingizini. Niliikasirikia sana sauti ile.Lakini usingizi ulinipitia, kwa mara nyingine,na swali lile lilijirudia,‘… mwisho wa ufariki wako na Remy utakuwa upi?’Mara hii, nilipatwa na hofu na kujiuliza,”…Ni nani huyu anayenitaabisha kwa kuniuliza swali hili?

Upanga Wa Ajabu Ndani Ya Glasi Ya Bia

Safari yetu ilikuwa ya tamasha la muziki iliyofanyika huko Dodoma.Tulipofika huko,nilijitenga kidogo na,baadaye, nilipoingia ukumbini,Ongala aliniagizia bia. Ajabu ni kuwa, kila nilipojaribu kuinywa,niliuona upanga wa ajabu ukiwa ndani ya bilauri. Hali ile ilinipelekea kukiacha kinywaji kile na kukimbilia nje!Siku iliyofuata, nilimwendea Ongala na kumweleza, ”… Rafiki yangu, mimi muziki basi tena. Ninarudi nyumbani, Dar es Salaam.” Ama kweli, matukio yote mawili:sauti na upanga, viliniogopesha sana!Sikuwa na furaha tena.Tuliagana na kuondoka.Remy, alipofika Dar es Salaam, alielekea BASATA na kuwaeleza yote yaliyotokea. Pia,  aliwaambia kwamba, kuanzia wakati ule, nisingeendelea na muziki, tena!

Maono Ya Ajabu Yanitokea

Mnamo mwaka 1993,kikiwa kimepita kipindi cha wiki moja toka nilipoachana na muziki,wenzangu walipata kibali cha kwenda kutumbuiza huko Marekani na Ulaya. Ongala,kwa kuwa alinipenda sana,alinifuata na kunishawishi ili, ikiwezekana, tuongozane katika safari ile.Nilishawishika na,nilipokuwa nikielekea Kinondoni-Studio,kuchukua nguo zangu Dry cleaner,sauti ile ilinionya waziwazi, “… Leo ndiyo mwisho wa maisha yako.” Nikiwa nimepigwa butwaa, bila kujua kilichokuwa kikiendelea,ghafla,nilishuhudia maono ya ajabu sana kutokea eneo la Magomeni, ‘Morogoro Road.’ Niliona   maono ya wazi wazi. Niliona mwisho wa pande za mpaka wa mbingu na nchi.Hili, nalo, lilinistaajabisha!

Ghafla nilihisi kuishiwa nguvu na,hata, ziliporejea kidogo na kuendelea na safari, sauti ile ile iliniambia, “… Hata nyumbani kwako hutafika. Utafia njiani.” Niliamua kujikokota hadi Magomeni, kwa mama mmoja,ilihali nikionekana mchovu na aliyekata tamaa ya maisha.Mama alinihurumia sana na kunikaribisha ili niketi,huku akiniuliza, ”… Mwanangu, kuna nini?” Nilimjibu, ”… Mama, ninakufa.”

Sheikh Anikataza Kupungiwa Majini

Yule mama aliamua kumuita Sheikh na, alipofika, alisema kuwa nilikuwa nimetupiwa jini. Baada ya taarifa ile tulielekea kwa Sheikh Mkuu, Abdala,ili kupungiwa mapepo.Lakini tukiwa njiani, sauti ile ilinionya kuwa kama ningefika huko ningekufa.Walijitokeza watu mbalimbali na kushauri kwa kadri walivyoweza.Sauti ile ile ilinijia, kwa mara nyingine, na kusema, ”… Nenda kanisani, huko utapata msaada.” Niliwaomba wale watu niliokuwanao wanipeleke kanisani na, ndipo, waliponipeleka KKKT,Kinondoni,kwa Mchungaji Fupe.Mchungaji alipotaka kujua kilichonisibu nilimjibu, ”nakufa.” Hayo yakitokea, niliishiwa nguvu ilihali sauti yangu ikiendelea kufifia.Nilitafuta pumzi kwa taabu huku, kwa mbali, nikimsikia mdogo wangu, Sadiki, akilia, ”kaka usifee!” Ghafla nilisikia radi iliyopiga kwa nguvu na kuzinduka nikiwa nimefunguliwa!Wale waliokuwa pamoja nami walisikia kitu kama mshindo mkuu! Baada ya tukio lile, mama mmoja alinipakia kwenye gari lake na kunipeleka kwa mtumishi mmoja wa Mungu aliyekuwa akiendesha semina pale Tanzania Assemblies of God(TAG) Kinondoni.Mtumishi yule aliponiona alisema, ”… Taarifa zako nilizipokea siku chache zilizopita. Nilipokuona tu, nikakukumbuka!” Toka siku ile niliamua kumfuata Yesu Kristo na, mpaka sasa, Mungu amenipa neema ya kuwa Mchungaji na nitamtumikia muda wote niwapo hai.

 

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *