CHARLES LUOGA

Gari Lililomgonga Laharibika Vibaya, Apona!

“…Kama atakuwa hajafa, basi, atakuwa ni jini aliyetumwa ili kutuangamiza lakini Mungu akatuponya. Kimsingi, nilichotarajia kukisikia kutoka kwako, kupitia simu nilipokupigia, ni kuwa umefariki! Lakini tuliposikia kuwa mgonjwa yuko hai, tena, nyumbani kwake, tulistaajabu sana! Mimi, mke wangu, na wote tuliokuwanao, hatukuamini!”

Mimi ni mchungaji wa kanisa la Tanzania Assemblies of God, Kongowe, Dar es Salaam. Ilikuwa tarehe 11. 05. 2006, mchana, nilipogongwa gari lililokuwa likitokea Ubungo, Riverside, kuelekea Mwenge. Niligongwa nilipokuwa nikikatiza eneo la kivuko cha waenda kwa miguu, Ubungo – Mataa, nikitokea zilipo ofisi za Makao Makuu (TAG), mkabala na Ubungo Plaza.

Kwa kweli, sikumbuki kama taa za barabarani zilituruhusu kuvuka mimi na wenzangu. Nikiwa katikati ya barabara, nilimulikwa na mwanga mkali wa gari usoni na, kuanzia hapo, nilipoteza fahamu! Nilipozinduka, nilijikuta nikiwa nimelala chini, katikati ya barabara, huku nimezungukwa na watu.Nilipoteza fahamu tena. Nilipozinduka, nilijikuta nikiwa ndani ya gari tukielekea Muhimbili. Hapo ndipo nilipotambua kuwa nilipata ajali na kuwatajia jina na taaluma yangu. Waliposikia nikizungumza, walipigwa butwaa! Wale ndugu walipogundua kuwa nilijitambua, waliniambia, “… Umegongwa na gari. Vitu vyako vyote hivi hapa.” Nilikabidhiwa fedha taslimu za Kitanzania(35, 600/-),simu, viatu, na briefcase! Nilipata maumivu makali. Nilikuwa na majeraha makubwa katika mkono wangu wa kuume. Niliwaomba wapige namba za mtu yeyote na, kwa nasibu, walimpata mdogo wangu.

Tulifika Muhimbili na, kwa mbali, nilisikia wakiwaeleza wahudumu (mapokezi) kuwa waliniokota, muda mfupi, baada ya kugongwa. Moyoni mwangu, nilisikia sauti ikiniambia, “Hawa ndiwo waliokugonga.” Kutoka hapo, nilipelekwa kwenye chumba cha mionzi huku nikiwa sijiwezi!

Vipimo vilionesha kuwa nilikuwa mzima. Mifupa haikuvunjika wala haikupata ufa. Daktari aliyenihudumia aliamini kuwa sikuwa nimegongwa bali gari lile lilinisukuma na kuniangusha chini huku tukio hilo likisababisha mkono na mguu wangu kujeruhiwa. Daktari alinitaka kusimama, bila mafanikio. Kila nilipojaribu, nilihisi maumivu makali sana mwilini! Mwanzoni, alidhani kuwa ninadeka na kutoa amri iliyomtaka msaidizi wake kunisimamisha. Aliniinua, na, niliumia sana. Nilipiga kelele! Baadaye, daktari alibadilisha mtazamo wake na kutaka nipelekwe MOI. Ghafla niliambiwa kuwa ndugu zangu, walioongozana na washirika wetu, walikuwa wakinitafuta.

Huko MOI, uchunguzi wa kitabibu ulithibitisha kuwa nilikuwa salama. Hakukuwepo na mfupa wowote uliovunjika wala kuchubuka! Mwili tu ndiwo ulionekana kuvimba. Aidha, upande ule wa kushoto, uliogongwa, ulipooza.Mguu na mkono,pia, havikufanya kazi sawasawa. Baada ya kunipa dawa, alinirejesha nyumbani. Hali yangu, kwa wakati ule, ilikuwa dhaifu kabisa.

Daktari, licha ya kupingwa na ndugu zangu, alisimamia maamuzi yake. Kufuatia hali ile, uongozi wa kanisa ulitaka kunihamishia katika hospitali binafsi. Hata hivyo, waliafikiana kuwa nibaki nyumbani, kwa muda, huku nikiangalia maendeleo yangu kiafya.

Mnamo siku ya tatu, nikiwa kwenye ibada ya maombi ya usiku, nilihisi kama niliguswa na umeme huku nikisikia sauti ikiniambia, “… Simama.” Na, kila, nilipojaribu kusimama,nilitiwa nguvu na kumtukuza Mungu. Siku iliyofuata,nilichechemea na kujikongoja mpaka kanisani. Niliendelea kupata nguvu na kuwashangaza wengi kwa hatua ile.

Uso kwa Uso na Aliyemgonga

Siku moja, nilipokea simu ya mtu aliyejitambulisha kuwa rafiki wa Mchungaji Luoga na aliyetaka kujua hali ya mgonjwa (yaani mimi) ilivyo. Nilimjibu kuwa mimi ndiye. Ghafla alikata simu!  Nilimjulisha, kwa mara nyingine, kuwa mimi ndiye. Simu yake iliendelea kuwa hewani, kwa zaidi ya dakika 1, bila majibu! Hapo ndipo aliponiuliza, “uko wapi?” Nilipomjibu tu kuwa nilikuwa nyumbani, alikata simu.

”… Ilipofika saa 11 za jioni, nilipokea simu, kupitia namba ileile na kunieleza waziwazi kuwa yeye ndiye aliyenipigiana na,kuwa, ndiye aliyenigonga! Pia, alitaka kujua kama nilikuwa mzima au la; au nilikuwa nyumbani au la! Nilimsimulia kuwa, baada ya kunitelekeza huko Muhimbili, Mungu alinisaidia! Mara, nilimsikia akishangaa, “Hakika Mungu yupo na, hata sasa, anatenda miujiza.” Ndugu huyu alisema kuwa alitamani kuonana nami. Tulipanga kukutana huko Muhimbili Hospital, Jumanne, siku niliyotakiwa kwenda huko ili kufanya tathmini ya maendeleo yangu ya kiafya.

Siku ile ilipowadia, niliambatana na mke wangu, dereva, na mzee wa kanisa. Tulikubaliana kuwa tungekutana katika eneo la mapokezi, MOI. Tukiwa mapokezi, ndugu yule alinitambua na, mara, alisema kwa sauti, “Hakika Mungu yupo hata siku za leo na anatenda makuu,” na, akielekea tulipokuwa, alitusalimia kwa furaha. Watu walipousikia ukiri ule, walishangaa sana na kutaka kujua kulikoni. Akiwashuhudia kilichomsibu, alisema, “Huyo mtu wa Mungu ameponywa kimiujiza.” Alipomaliza simulizi ile, alinichukua na kuniingiza katika chumba cha daktari.Hapo ndipo nilipotambua kuwa niligongwa na daktari. Akizungumza na madaktari wenzake, aliagiza kuwa nifanyiwe uchunguzi wa kina ili kubaini kama nilikuwa mzima au la!

Uchunguzi wa madaktari ulithibitisha kuwa nilikuwa mzima.Hata sehemu ile iliyoonekana kuvimba, hapo awali,ilirudia hali ya kawaida. Baadaye, tuliamua kutafuta eneo zuri la kukaa ili aweze kutusimulia namna ajali ile ilivyotokea. “… Mlikuwa mkivuka barabara. Wakati huo, taa za njano,iliyoruhusu magari kuendelea, ikiwaka. Wewe,ukivuka, ulinusurika kugongwa na gari moja. Ulikwepa kwa kurudi nyuma na, kwa bahati mbaya, nikakugonga. uliangukia juu ya boneti na kutua barabarani, upande wa kulia unapotokea River Side.Uligongwa na gari aina ya Mistubish – Double Cabin, lililokuwa na ngao kwa mbele. Baada ya kugongwa, vyuma vilivyounda ngao za gari lile zilipinda na kuvunja shoo ya mbele, karibu na rejeta.”

Daktari Azungumza

Nilishangaa sana kusikia kuwa mchungaji Luoga alikuwa hai. Wote tulioishuhudia ajali ile, ilipotokea, tulistaajabu. Nilipowaambia kuwa yule tuliyemgonga ni mzima wa afya, hata wao, hawakuniamini. Wengine waliamini kuwa aliyegongwa alikuwa jini. Hili ndilo lililonipelekea kukutafuta ili kujiridhisha.Ili kumthibitishia Mchungaji kuwa nilimaanisha nilichokisema, nilimuonesha jumbe fupi za maandishi, nilizotumiwa na wenzangu. “…Kama huyo mtu hakufa, basi, hatukumgonga binadamu wa kawaida; tulimgonga jini, alitumwa ili atuue. Ashukuriwe Mungu kwa kutuponya,” alisimulia na kuendelea, “… Kimsingi, nilichotarajia kukisikia kwako, siku ile nilipokupigia, ni kuwa umekufa!Hakika, Mungu ametenda muujiza mkubwa kuliko tulivyolichukulia suala hili!”

Pia, nilimwomba mchungaji na ujumbe alioambatana nao, ili twende tukalione gari lililomgonga.Ilikuwa bahati kuwa, siku ile, niliruhusiwa kuliondoa gari lile kutoka katika himaya ya Polisi, liliposhikiliwa toka siku ile tulipopata ajali.

Mchungaji na ujumbe wake, walifika na kulishuhudia gari lile likiwa limebondeka sana. Walishangaa sana na kujiuuliza, “… Hivi, inawezekanaje kwa gari lililogonga kuharibika vile, ilihali aliyegongwa akiwa mzima? Pia, walishangazwa na taarifa kuwa, katika hali ile, lilinyooshwa ili, walau, kulifikisha gereji! Walipotambua kuwa Mungu alimnusuru Luoga na mauti, walishangaa! Gari lenyewe lilikuwa limebomoka. Sehemu ya chini ilishinikizwa kwa bolti na nati, ikiungwa kwa nyaya. Ndugu hawa, walipopata ufafanuzi ule, ndipo walipotambua kwa nini nilimtukuza Mungu nilipowaona kwa mara ya kwanza.Ni Mungu pekee aliyemnusuru Luoga na kuhifadhi mifupa yake isivunjike!

Polisi Amshangaa Aliyegongwa!

Tulikwenda mpaka kule gari liliposhikiliwa.Tukiwa huko, askari aliyelikagua gari lile alishangaa sana alipoona namna gari lile lilivyokuwa limeharibika! Pia, alishangaa sana aliponiona nikiwa mzima. Hakuamini kuwa niliruhusiwa kutoka hospitalini na. Kwa sababu hiyo, alimtaka dereva (daktari) aliyenigonga anipeleke kituoni kwake na, tulipofika, aliuliza, “… Ati huyu ndiye yule uliyemgonga?” Dereva yule aliitikia, “Ndiyo. Huyu ndiye.”Baadaye, aliomba nimsimulie namna nilivyogongwa na, ikiwa nilijua jambo lolote lililojitokeza. Nilieleza kilichotokea kule Muhimbili, vipimo, na kule nyumbani. Naye, polisi, baada ya kuyapitia maelezo yangu, aliuliza kama ningekuwa tayari kumshitaki aliyenigonga na, ndipo, nilipomhakikishia kuwa sikuwa tayari. Polisi aliandika maelezo yangu na kunipa ili niyasome kabla ya kuweka saini yangu.Huo ndiwo uliokuwa mwisho wa shauri lile!

Jambo la Kuzingatia

Mimi nimekuwa shahidi wa matendo makuu ya Mungu. Nimelisoma na kuliishi neno lake. Nimemuona Mungu akinitendea na kuwatendea wengine.Pia, nimewaona watu mbali mbali, katika huduma yangu na kwingineko, wakiendelea kuukulia wokovu. Kupitia muujiza huu, pendo na utumishi wangu kwa Mungu vimeongezeka. Ninataka nikuhakikishie wewe, unayeusoma ushuhuda huu, kuwa Mungu yupo. Anatenda miujiza, huwalinda watu wake, na kuwaponya!

 

 

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *