BAYOMBYA MADULU NDAKI

  • Jambazi aliyefungwa miaka 27 jela, akakutana na Yesu.

Nilipigwa risasi mgongoni, tumbo likafumuka, utumbo wote ukatoka nje, lakini  kwa rehema za Mungu, nikapona. Wenzangu wanne niliohukumiwa pamoja nao, walifia gerezani, mimi peke yangu, nimeokoka na sasa niko huru  kuhubiri habari njema.”

 

Nilizaliwa Januari 8 mwaka 1967 katika kijiji cha Msisi Sarrale, Tarafa ya Serengeti Wilaya ya Bunda Mkoa wa  Mara. Natoka katika kabila la Wasukuma  familia ya  wapagani, inayoamini mizumu. Baba yangu mzee Madulu, alikuwa na wake wengi sana.

 

Nilihitimu elimu ya msingi Mwaka 1982, lakini baada ya kuhitimu darasa la saba, sikuweza kuendelea na masomo ya Sekondari, nilibaki nyumbani nikichunga mifugo, kwani baba yangu hakuwa na desturi ya kuwaendeleza watoto wake kupata elimu.

Miaka miwili baada ya mama yangu kufariki dunia kaka yangu aliyekuwa mwanajeshi alikuja na kunichukua kuja kuishi naye Dar es Salaam.

 

Baada ya kufika jijini Dar es Salaam, kaka alinitafutia kazi katika kampuni moja ya ujenzi na kwa kipindi hicho mwaka wa 1984 hali ilikuwa ngumu sana baada ya taifa kutoka katika vita ya Kagera.

Kutokana na hali hiyo nililazimika  kuanzisha biashara ndogo ndogo (machinga) pale mtaa wa Lumumba. Nikiwa katika biashara hiyo huku hali ya maisha ikiendelea kuwa ngumu, ndipo nilipokutana na vijana wenzangu wabaya (majambazi).

Vijana hao ambao tulikuwa rika moja na mimi walionekana wenye mafanikio makubwa kimaisha kuliko mimi, hivyo nikatamani kuwa kama wao.

Pasipo kujua tabia yao, nilijiunga nao na kuanza kidogo kidogo kutafuta pesa pamoja nao kwa njia ya wizi na baadaye kuja kuwa jambazi.

Katika kutafuta pesa huko siku moja tulimtembelea kiongozi wetu mkuu, mitaa ya Ubungo, ndipo  tulipozingirwa na polisi na mimi nikapigwa risasi ya tumboni iliyosababisha utumbo kumwagika nje.

 

Kutoka hapo sikujitambua hadi nilipozinduka baada ya wiki mbili na kujikuta niko chini ya ulinzi wa askari katika hospitali ya taifa ya  Muhimbili.

Nakumbuka baada ya matibabu, nikiwa bado ninahisi maumivu makali nilifikishwa mahakamani hapo nilisomewa hukumu na kufungwa miaka 27 katika gereza la Keko jijini Dar es Salaam hapo ilikuwa tarehe 21 Juni 1980. Ilipofika Januari 3 mwaka  1991, nilipohamishiwa gereza la Ukonga.

Tarehe 10 Novemba mwaka 1991 Nikahamishiwa  gereza la Luanda Mbeya. Na Februari 1992 nikahamishiwa tena Songwe. Ilipofika Septemba mwaka huo huo, nilihamishiwa Morogoro mjini. Mwaka 1994 February nilirudishwa tena katika gereza la Ukonga.

Nakumbuka wakati naingia gerezani nilikuwa na majeraha ambayo hayakupona haraka. Na huko nilikutana na mzee Eliya aliponiona alinikabisha kwenye darasa lake la mafunzo ya neno la Mungu, akanipenda kwakuwa nilikuwa mwepesi wa kushikilia mambo.

Mwaka 2004 niliota ndoto nikamweleza Sheikh, waliokuwa katika gereza hilo, wakashindwa kunifasiria. Baada ya siku tatu nikaitwa na mkuu wa gereza akanielekeza kuwa, kuna amri imekuja nipelekwe kwenye chumba cha mateso.

Amri ya kupelekwa kwenye chumba cha mateso ilikuja baada ya mimi kuandika barua ya malalamiko kwa Kamishina wa gereza kusu wafungwa kunyolewa upara kwa kutumia wembe moja. Jambo ambalo lingehatarisha maisha yao kutokana na magonjwa ambukizi kama Ukimwi.

Nikapelekwa huko lakini ile ndoto iliendelea kunisumbua nikiwa huko niliota ametokea mtu mmoja na kunipa Biblia. Ndoto ikaja kuwa kweli baada ya mtu mmoja kuniniletea Biblia mle chumbani na kuniachia.  Katika kusoma ile Biblia akaja askari mmoja kutoka Mbeya alileta wafungwa na alikuwa akitembelea vyumba ndipo alinikuta nikisoma.

Tulianza mazungumzo, nikamweleza ile ndoto, kumbe alikuwa ameokoka, baada ya kumsimulia ndoto nilizoota alinitafriria.

  • NDOTO ZA NDAKI

Niliota natembea mahali fulani nyumbani kijijini kulikuwa na mti niliokuwa nauendea lakini kabla sijafika kwenye ule mti nikajikuta niko kwenye korongo.

Nikakuta wafungwa wanagawana nyama mbichi, nikaondoka nikimbie nikakutana na mafuriko yanapiga kelele mbele yangu.

Nilipokuwa nakimbia niwaokoe wenzangu maji yakawa yamenifikia, bahati nzuri nikaona kisiki niliposimama kukiangalia vizuri nikaona mlima na kusikia mtu akiniita.

 

Ndoto nyingine ni ile niliyoota nikiwa katika chumba cha mateso gerezani, ambapo nilionyeshwa nikiwa katika pori kubwa, ghafla nikaona kichaka kikubwa ndani yake alitoka nyoka mkubwa akawa akinifuata. Wakati nakimbia alitokea mtu akiwa amevaa kanzu ndefu akanipa upanga na kuniambia nimuue yule nyoka. Nakumbuka katika ndoto hiyo nilimuua huyo nyoka.

Na baada ya siku chache nikatolewa katika kile chumba cha mateso.Tarehe 16 Novemba 2004 nilipata neema ya kukutana na Yesu, na kuokoka.

Tangu siku hiyo  nilianza kuhubiri ijnjili kwa wafungwa wenzangu, nikiwa gerezani na siku ya kwanza waliokoka watu zaidi ya 20.

Tangu 2004 hadi leo katika injili niliyofanya watu zaidi ya 2000 wamempa Yesu maisha yao.

NDUGU, MGANGA WAMALIZA MSIBA WANGU

Kumbuka kwamba nilipohukumiwa ndugu zangu walifanya tambiko la msiba ili kufuta jina langu ktika uso wa dunia baada ya mganga kuwaambia kwamba sitatoka wala mazishi yangu ya mwili wangu hayataonekana.

Kwa maana hiyo maisha yangu yalifutika katika kumbukumbu za ndugu zangu,  baada ya tambiko hilo. Tangu wakati huo hakutokea   ndugu hata mmoja aliyethubutu kunifuatilia kwa takribani miaka 20. Nakumbuka baada ya miaka kadhaa ndugu yangu mmoja aliyekuja jijini Dar es Salaam, kwa masomo alichukua hatua ya kutaka kujua kama bado niko hai. Huyo ndiye aliyeniibua kisa cha uhai wangu kwa ndugu wengine, baada ya kuelezwa na wakuu wa magereza kuwa niko hai. Ndugu huyo alilazimika kutoa taarifa  kwa ndugu wengine kwamba, niko hai na kufanya sasa waanze kunifuatilia kwa ukaribu zaidi. Nakumbuka nililetewa taarifa za kufariki kwa baba yangu, na ndugu yangu mmoja aliyekuwa akifanya biashara ya kusambaza vyakula kwenye gereza mojawapo huko Mwanza, kupitia kwa wakuu wa magereza. Baada ya taarifa hiyo walitaka kufahamu natoka lini, ndipo nilipowaambia kuwa bado nimesaliwa na mwezi mmoja tu nitoke.

Baada ya kupata taarifa hiyo walirudi kwa mganga wao yule aliyewafanyia tambiko la kumaliza msiba wangu, wakamweleza uwepo wangu, na kwamba siyo hivyo tu, bali nimesaliwa na mwezi mmoja tu nirejee nyumbani.

Mganga akawaambia, kwakuwa limetokea jambo  hilo, basi inabidi wafanye tambiko lingine la pili la ukombozi kwa ajili ya kufuta lile la kwanza. Wakati huo Mungu alikwisha nijulisha yote yanayopangwa dhidi yangu. Aliwaagiza waandae nguo maalum ya kunivika pamoja na dawa ya kuniogesha pindi nitakapotoka gerezani.

Kwa neema ya Mungu nilitoka gerezani mwaka 2017 na ndugu zangu waliposikia kwamba niko huru,  walipanga kunifanyia tambiko kama walivyoelezwa na mganga wao wa jadi. Walinitumia mjumbe kuja kunipokea jijini Dar es Salaam, akiwa na kila kitu kama alivyoaandaliwa na mganga wa jadi, huku ndugu wakinisubiria Mwanza. Aliponieleza sikukubaliana nao kwasanbabu mimi tayari nilikuwa mtu mwingine  nimeokoka.

Nilimwambia ndugu yangu aliyetumwa kuniletea dawa, “naomba uelewe kabla sijaingia gerezani nilikuwa natoka katika mazingira ya mizimu ya babu, nilikuwa simjui Mungu,  lakini kwa sasa namjua na amenibadilisha maisha yangu. Siko tayari kutumia dawa hizo maishani mwangu.” Sambamba na hilo pia walikuwa  wameniandalia mavazi na mke wa kuoa.

Baada ya majibu hayo, ndugu yangu huyo aliondoka bila kuniaga na kuniachia bila nauli, nikatangaziwa vita na familia, hata peza walizochanga kunizawadia wakaghairi. Nililazimika kwenda kwa Askofu Pengo, ambaye alikuwa na taarifa zangu kutoka kwa Padre mmoja aliyetutemdelea  gerezani  huyo ndiye aliyenipa Shilingi 150,000, zilozonisaidia kusafiri kwenda Mwanza.

Mimi namshukuru sana Mungu, kwani gerezani tulihukumiwa watu watano (5) katika kesi hiyo moja, wenzangu wanne (4) walifariki. Baada ya hapo, niliweka nadhiri kwamba “kama Mungu atanitoa nikiwa salama, nitamtumikia.”

Mungu ni mwaminifu amenitoa na amenipa mke mwema tunamtumikia Mungu pamoja.

  • MATARAJIO

Najisikia faraja kwamba hata kama nilihesabiwa nimekufa lakini Mungu ameniweka hai. Lakini pia Mungu amenipa mke mzuri na sasa namtumikia Mungu katika kanisa la VCC Ngeta mlandizi. Natarajia kuwa na huduma ya kuwafikia wafugwa magerezani.

Niwaase vijana ambao wanachipukia kuepuka maisha ya tama ya mali za haraka, pia waepuke makundi maovu, badala yake wajikite kufanya kazi kwa kufuata sheria za nchi, na uadilifu. Na pia wamgeukie Mungu katika maisha yao awaepushe na tama mbaya. AMINA

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *