WATENDE KIYAGI

Mtoto wa Mitaani

‘Sikuweza kumaliza shule kwa sababu ya ukata ulioikabili familia. Kila nilipopelekwa shuleni, nilitoroka. Nilitorokea visiwani, machimboni na, hata, mijini nikitafuta namna ya kuikwamua familia ili tuondokane na umasikini. Kupitia kutafuta huku, hatimaye, Maisha yangu yakawa ya mitaani. Nilidharaulika, jamii ilinitelekeza na kuonekana kama mtoto asiyefaa. Lakini Mungu, kwa wingi wa rehema, amenufanikisha. Ninamiliki kampuni, nyumba, na magari kadhaa hapa hapa Dar es Salaam.

 

Nilizaliwa tarehe 07 July, 1978 huko Isimani, katika Wilaya ya Iringa Vijijini, nikiwa mtoto wa kwanza katika familia ya Mzee Kiyagi, nakifungua mimba miongoni mwa wajukuu wa Mzee Mpogole, aliyekuwa mganga wa kienyeji maarufu sana huko Isimani. Aidha, babu alijulikana, pia, kwa jina la utani, Mzee Muhimbili. Alipachikwa jina hili kulingana na shughuli alizozifanya: uuguzi na kulaza wagonjwa waliosumbuliwa na maradhi mbalimbali, ukichaaukiwemo. vichaa, wakiwa katika himaya yake, walifungwa kwa minyororo. Hali hii iliyopelekea babu kuitwa ’Muhimbili.

 

Nimekuwa katika maisha ya kutangatanga toka nikiwa na umri mdogo sana, miaka minane tu! Na, licha ya kupendwa sana na babu, sikutulia nyumbani. Nilipuuzia masomo na kuamua kuwa mtu wa kuzungukazunguka:visiwani,machimboni,na, hata,mijini.Nakumbuka,kuna wafanya biashara fulani walinichukua na kunipeleka katika kisiwa kimojawapo cha bwawa la Mtera na kunitelekeza huko. Kwa muda wote wa miezi sita niliokaa huko,nikifanya kazi ya  kubanika samaki wao, sikuonana na mtu yeyote.Walikuja na kuwachukua samaki niliowabanika na kuondoka nazo huku wakiacha, hapo hapo, nikiwa mpweke.Pia, hawakuniachia kitu chochote isipokuwa unga, chumvi na samaki wachache!

 

Niliendelea kuwa katika hali ile mpaka nilipougua na kusaidiwa na wavuvi waliopita karibu kabisa na nilipokuwa. Walipoitikia wito wangu, niliomba wanipeleke nchi kavu ili, ikiwezekana, nipate msaada wa matibabu! Kweli, watu wale walikuwa wasamaria wema kwa kuwa walisafirisha, kwa mtumbwi, mpaka nchi kavu. Huko nilibahatika kukutana na watu walionitambua. Ajabu ni kwamba, nilipoteremka tu kutoka kwenye mtumbwi, malaria ilipanda kichwani. Kuona vile, na, kwa kuzingatia hali niliyokuwa nayo, wale ndugu walitumia mkokoteni kunisafirisha mpaka stendi ilihali nimefungwa kamba. Tulibahatika kupata lori lililonisafirisha na kunifikisha nyumbani saa saba za usiku.

 

Tulipofika dereva alipiga honi ili kuwaamsha wazazi wangu ambao, nadhani, walilala fofofo! Na, kulingana na maelezo waliyopewa na wale wasamaria wemamwalionisafirisha na tulioishi nao katika kijiji kile, walinichukua na kunipeleka kwa babu Muhimbili. Wakati wote huo, nilipiga kelele na, wala, sikujielewa. Kwa hiyo, ilinibidi kukaa kwa babu, huku nikiaguliwa, mpaka nilipopona kabisa.

 

Zilipotimu siku tatu tu, baada ya kupona, nilirudishwa shuleni ili kuendelea na masomo. Walifanya hivi kwa kuwa, kila niliporudishwa shule, mara zote, niliondoka bila kuaga. Kwa kuwa nililazimishwa, nilisoma kwa muda wa miezi mitatu (3) na kuondoka kwa miguu, usiku mmoja, kutoka kijijini kwetu mpaka Iringa mjini. Huko nilikutana na mama mmoja aliyenichukua na kunipa kibarua cha kumuuzia mayai. Kazi hii ilinifanya kuwa mithili ya kijana aliyeishi stendi. Niliifanya kazi ile kwa uaminifu na, baada ya miezi mitatu, nililipwa mshahara wangu na, niliamua kurudi nyumbani.

 

Kama kawaida, nilipoonekana tu nilirudishwa, tena, shuleni na kufanikiwa kusoma kwa muda wa miezi miwili hivi. Kwakweli, kama nilivyoyachukia maisha ya nyumbani, kadhalika niliichukia shule. Nilikaa nyumbani kwa muda na, nilipojiridhisha kuwa maisha yetu yalikuwa duni sana, nilitoroka na kurudi tena mjini. Nikiwa huko niliijiwa na wazo la kwenda Tunduru, nikitamani sana kwenda machimboni. Wazo hilo liliponiijia, sikuwa na nauli ya kunifikisha huko. Niliwaza na kuwazua huku nikitafuta namna ya kufanya.

 

Hatimaye, niliamua kuchukua viroba vya sukari na kuvijaza kwa mchanga, kuvibeba na kuvipeleka stendi. Huko nilimkabidhi kondakta wa gari na kumuomba aupakie mchele (asijue kuwa ule ulikuwa ni mchanga) mpaka Njombe na gharama za usafirishwaji kulipwa huko huko. Yule kondakta hakunikatalia. Aliuchukua mchanga ule, akaupakia na, kuanza safari na kufika Njombe jioni sana. Nilianza kutafakari namna ya kushawishi kondakta na kupata wazo la kumwambia,’Ninafuata hela za kukombolea mzigo, nikitafuta mwanya wa kumponyoka bila ya kunistukia! Alikubali na, ndipo, nilipoondoka na kuanza kuwaulizia watu ili wanioneshe yalipo maegesho ya malori ya mizigo ya kuelekea Songea. Nilimpata mtu mmoja aliyenionesha eneo lile nami nikaenda nikaenda na kukaa huko nikiwa abiria waliokuwa na mizigo ama waliokuwa wakisubiri magari ya kuwasafirisha, wao na mizigo, mpaka Songea.

 

Usiku ule ulikuwa na baridi kali. Hali ile ilitulazimu kukoka moto, kama saa saba hivi usiku, kabla ya kuja kwa lori (semi-trela), iliyomilikiwa na Iringa Retco, na kupakia mizigo yote iliyokuwepo eneo lile. Mimi, kwa kuwa, sikuwa na nauli, nililazimika kukaa tu mpaka shughuli ilipomalizika. Niliamua kulirukia gari, lilipokuwa likianza kuondoka, na kukaa katika eneo hatari lililotenganisha gari na tela lake. Eneo hili lilikuwa na gurudumu la ziada na, nililotumia kama kiti, kusafiri usiku wote, mpaka Songea. Tulifika huko majira ya saa kumi na moja za jioni na, gari lilipoanza kupunguza mwendo, nilishuka na kuanza kutembea kwa miguu kuelekea nisikokujua.

 

Safari ile ilinifikisha katika kituo kimowapo cha mabasi. Huko nilitaka kujua kama ningalipata basi la kwenda Tunduru. Kwa bahati nzuri, niliwakuta mafundi, kadhaa, wakilirekebisha gari nililokuwa nikilitafutana na, ndipo, nilipoanza kuwasogezea vifaa (spana, vitambaa vya kufutia n.k.,) mithili ya fundi mwenzao. Ubunifu ule uliwapelekea kunizoea, kwa muda mfupi, na kuondoka wote. Awamu hii, nilidhamiria kufika Tunduru (Machimboni). Kwa sababu ya ubovu wa barabara, tlilazimika kutumia siku tatu tukiwa njiani. Kwa kweli, tuliteseka sana! Wakatiwote, kabla ya kufika Tunduru, tulikula vyakula vilivyopakiwa na wateja.

 

Tulifanikiwa kufika Tunduru salama na kuanza kuulizia eneo la machimbo. Nikiwa huko, niliambatana na rafiki aliyekuwa mzoefu wa mazingira yale na kuishi naye kwa muda wa wiki tatu. Kwa bahati, jamaa yule alipata madini na, ghafla, tulianza kuzifuja pesa zile. Siku moja tuliondoka naye mpaka Songea na kuanza maisha ya anasa. Tukiwa huko, tuliishi kwenye nyumba za wageni huku tukilewa na kufanya starehe zinginezo mpaka pesa zikaisha.

 

Baada ya kuachana na ndugu huyu, nilikutana na jamaa yangu, tuliyefahamiana kuanzia nyumbani, na kunikaribisha nyumbani kwake. Nikiwa kwake, tulifanya biashara ya kuuza mitumba. Kwa nasibu, siku moja, nilikutana na dada mmoja (kutoka nyumbani) na niliyemuita mama mdogo. Mama huyu (Grace Ngoda) na mumewe (Cheichei), walinichukua ili nikawasaidie kuuza katika duka walilolimiliki huko Songea. Niliifanya kazi ile kwa uaminifu, kwa muda wa miezi mitatu, na, ulipotimu msimu wa kilimo, alinipeleka katika shamba lake lililokuwa Mtangimbole na kufanya kuwa msimamizi wa mashamba yake. Kwa kweli, maisha yale yaliniwia magumu na, ndipo, nilipomuomba ili, ikiwezekana, aniruhusu kurudi nyumbani.

 

Ninamshukuru Mungu kuwa hakunikatalia. Nakumbuka, niliondoka, kesho yake, asubuhi na kuanza safari ya kurejea nyumbani. Wazazi wangu walifurahi sana waliponiona. Kama kawaida yao, walinirudisha tena shuleni ili kuendelea na masomo. Nilikuwa mtoto mgomvi na, kwa kweli, sikupenda mazingira yoyote yaliyohusiana na kusomasoma! Nilijilazimisha kwenda shule na, ulipomalizika muda wa mwezi mmoja hivi, nilianza kufanya kazi za ukondandakta katika magari yaliyotoka kijijini (kwetu)kwenda mjini. Niliendelea na kazi ile kwa muda wa miezi minne na, taratibu, niliiacha na kujiingiza kwenye magari makubwa (yanayobeba samaki kutoka katika bwawa la Mtera kuelekea Songea na Mbeya), kwa miezi sita, kabla ya kuhamia kwenye mabasi ya King Cross!

 

Nikiwa King Cross, magari yaliyokuwa yakitoa huduma zake kati ya Mtera na Dodoma, nilidumu kwa mwaka mmoja tu na kuamua kurejea nyumbani! Huko, kwa kuwa sikuwa na kitu cha kufanya, nilijikuta nikimsaidia mama mmoja – Mama Hakimu – kazi za nyumbani!

 

Ninamshukuru Mungu kuwa, mimi nilyedharauliwa na kukataliwa na watu, wakiniona kuwa mtu asiyefaa, leo hii, baada ya kumpokea Yesu na kufanyika Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, ninamiliki familia nzuri, nyumba ya kuishi (hapa Dar es Salaam), kampuni, na magari kadhaa. Ninakushauri ndugu yangu, unayeusoma na kuusikiliza ushuhuda huu, kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kumkabidhi Mungu maisha yako! YEYE ndiye Mhusika Mkuu katika maisha yako muda wote uwapo hapa duniani. Kwanini uteseke ilihali msaada ungalipo?

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *