DK. JOE MZIWANDA (Kiongozi wa Dini)

“Mafanikio  bila Mungu sawa na kujilisha upepo. Ni kuwa na furaha bila amani ya kweli. Niliishi maisha ambayo, licha ya kuwa yenye furaha, sikupata amani ya moyo. Hii ilinipelekea kuwaza sana siku moja na, hatimaye, niliamua kuchukua maamuzi sahihi. Maamuzi yale ndiyo yaliyoniwezesha kupata amani iliyoambatana na furaha niliyoitafuta kwa muda mrefu.”

Historia Yangu

Mimi nilizaliwa mnamo mwaka 1952, katika kijiji kimoja kidogo sana kilichokaliwa na idadi ndogo ya wakulima huko mkoani Morogoro. Nilibahatika kuwa mtoto wa mwisho katika familia ya wakulima yenye watoto 10. Huu ndio ukweli ninaoweza kuueleza kuhusu maisha yangu. Nilitokea mahali fulani, tena, katika maisha yaliyokuwa duni kuliko unavyodhania. Hata hivyo, mazingira yale hayakuweza kubatilisha maono yangu ya muda mrefu toka nikiwa na umri mdogo kabisa. Nilikuwa na maono ya kuwa mfanyabiashara mkubwa na mwenye mafanikio ya hali ya juu. Hii ndiyo ilikuwa shauku yangu toka utotoni!

Elimu na Maisha, shauku iliyonifikisha kwenye maendeleo makubwa

Kama walivyo watoto wengi wanaotoka katika mazingira ya kimasikini, nilijpatia elimu ya msingi mpaka sekondari. Baadaye, nilijiendeleza na kujipatia astashahada ya uhasibu kutoka katika chuo cha biashara cha CBE. Hata hivyo, niliendelea kujisikia mtupu! Ilikuwa dhahiri kuwa sikuwa nimekipata kile nilichokihitaji. Baada ya kuhitimu, nilibahatika kupata kazi ya uhasibu katika kampuni ya Williamson Diamond. Licha ya kuifanya kazi ile kwa uaminifu mkubwa niliendelea kuhisi na kuamini kuwa nilipaswa kuyaishi maono yangu ya kuwa mfanya biashara mkubwa hapa nchini na, ikiwezekana, katika ukanda wote wa Afrika Mashariki.

Shauku ile ilinipelekea kurudi, tena, chuoni. Mara hii, nilijiunga na chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Nilisoma kwa bidii na, ilipofika mwaka 1977, nilibahatika kupata ajira, niliyoitumikia kwa muda wa miaka 10, kupitia kampuni ya Leopold Wallfaer Uk., Nikiwa katika utumuishi ule, bado, nilitamani kuwa mfanya biashara mkubwa kama nilivyotangulia kusema. Nilikuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha. Hali ile ilinisaidia sana kutobweteka kama ilivyokuwa kwa vijana tuliokua nao pamoja,  Nilitekeleza majukumu yangu kupitia nafasi yangu na, ilipofika mwaka 1986, nilifanikiwa kuanzisha kampuni yangu binafsi na iliyojulikana kama JAMBO FREIGHT LTD. Huu ulikuwa mwanzo wa utimilifu wa ndoto niliyotamani kuitimiza toka nikiwa mtoto mdogo kabisa!

Mabadiliko yenye tija, yaliyonipa amani ya kweli maishani

Niliendelea kuisimamia kampuni yangu huku nikipambana na mazingira ya kazi, kama yalivyojitokeza. Pia, nilijua kuwa, bila kumhusisha Mungu katika yote ninayoyafanya, hakika, nisingalifikia upeo wa mafanikio niliyoyahitaji. Hivyo, siku moja, niliamua kuokoka baada ya kuyatafakari maisha yangu kwa upana wake. Hii ilikuwa mwaka 2004. Kwa kweli,  sikutaka kuwa na wokovu nusu. Mimi, tofauti na vijana wengi siku hizi, niliamua kuokoka, mimi na kampuni yangu kadhalika! Nilipoongozwa sala ile ya toba na kumkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, nilifanya vile nikijua kuwa kampuni yangu ilijumuishwa kupitia ukiri ule. Niliamua, kuanzia wakati ule, kuendesha shughuli zangu kwa kuzingatia kanuni zote za Kibiblia. Niliamua kuachana na pombe na starehe zote nilizokuwa nikiziendekeza hapo kabla! Niliamua kulifunga duka langu la kuuza pombe lililojulikana kama Bahama Mama Club. Ni mkazi yupi wa Dar es Salaam hakuwahi kuifahamu baa ile? Niliamua kuacha vyote. Niliamua kuambatana na Kristo, toka moyoni na, mtazamo huu, ulinipa amani ya kweli kutoka Juu!

Maamuzi yangu  kubadili Baa kuwa nyumba ya ibada

Ile tabia ya kuendesha fellowship (ushirika), huku nikishughulika na shughuli za kuuza pombe niliitokomeza.  Ili kuithibitisha imani yangu, nilipookoka niliifunga Bahama Mama Club na kulitumia jengo lile kwa shughuli za ibada chini ya kanisa la Beloya Bible Fellowship Church (BBFC) lililopatikana katika eneo la Kimara Baruti. BBFC ilianzishwa mnamo mwaka 2015 na, mpaka sasa, linalokadiriwa kuwa na zaidi ya waumini 150.

Ninapenda kuwaasa Watanzania, na yeyote atakayeusoma ushuhuda huu, kuwa unaweza kuwa na furaha ya kitambo tu kwa kutomhusisha Mungu katika biashara yoyote unayoifanya. Hata hivyo, furaha hiyo haitakupa amani ya kudumu, kama shughuli hiyo haikujengwa kwenye msingi imara wa Neno.

Maisha Yangu kwa Sasa

Maisha yangu yamejaa amani ya kutosha. Ninajisikia kuwa na amani ya kutosha, tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuokoka, kwa sababu biashara na kazi ninazozifanya zinamtukuza Mungu! Ukiacha kazi yangu ya kulisimamia kundi, ninamiliki biashara za Logistics (usafirishaji) ninazoziendesha kupitia Yard kubwa iliyopo hapa hapa Dar es Salaam, barabara ya Pugu. Pia, Mungu amenizawadia mke (Elizabeth Joe Mziwanda), na watoto wanne,  Jambo la kumshukuru Mungu ni kuwa ndoa yetu ina amani ya kutosha!

 

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *