Mwimbaji wa Nyimbo za Injili
“… Kupitia muziki, nilijipatia marafiki wengi sana, akiwemo Idd Amin Dadaa, kabla ya kumpindua Milton Obote na kuutwaa Urais wa Uganda! Baada ya kumpokea Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, niliamua kumtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji.”
Historia Yangu Kwa Ufupi
Mimi nimezaliwa January 28, 1940, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC).
Nilijiunga na elimu ya msingi na kubahatika kuendelea na shule ya upili! Nlitakiwa kuchagua kati ya Ualimu, Kilimo, na Umisheni, kama ilivyoelekeza sera ya elimu.Nilijiunga na seminari ambako tuliandaliwa ili,panapo majaliwa, tuweze kutumika katika nafasi mbalimbali za kikuhani kupitia kanisa Katoliki. Lakini, siku moja, tukiwa shuleni,tulipokea taarifa za kuuawa kwa aliyekuwa rais wetu, hayati Patrick Lumumba, kwa kupigwa risasi, huko Kinshasa!Katika machafuko yale watu walipigwa, akina mama (wakiwemo watawa)walibakwa na kuuawa. Hata hivyo, niliendelea na masomo yangu mpaka mwaka 1962,kabla ya kukimbilia Uganda.
Nikiwa huko nilikutana na profesa Mazrui kutoka Tanzania Visiwani. Tuliamua kuambatana kama marafiki waliopendana!Kwa kweli, uhusiano wetu uliimarika na kumpelekea profesa kujitolea kunifundisha lugha ya Kiswahili.Nilijifunza na, haukupita muda mrefu, ubalozi wa Ubelgiji, nchini humo, uliridhia kututambua kama wakimbizi wa kisiasa.
Maisha Yangu Huko Italia
Mnamo mwaka 1964, nilibahatika kuitembelea Italia. Nikiwa huko, niliabudu katika jiji la Vatican, makao makuu ya kanisa Katoliki duniani (almaarufu jiji la Mapapa). Mwanzoni, niliamini kuwa eneo lile lilizingirwa na uwepo wa Mungu. Nilishangaa sana nilipowaona watu mbalimbali wakiuza dawa za kulevya (cocain na heroin) huku wakionesha kulemewa na hulka za kimapenzi! Hakika, hali ile iliniumiza sana.Niliutumia mwaka mmoja, niliokaa huko, kwa kujifunza lugha ya Kiitaliano huku nikiendelea na uimbaji na, ilipotimu mwaka 1965, nilirudi Uganda.
Nikiwa huko, nilifikia katika hoteli iliyomilikiwa na Muitaliano, Apollo Hotel. Baada ya muda, niliunda bendi ya muziki, Jambos na kupewa jina ’Mzee Makassy’. Pia, nilikutana na Idd Amini Dadaa, akiwa Kapteni wa jeshi. Tulikuwa marafiki walioshibana. Katika mkesha mmoja ulioendeshwa na bendi yangu, panapo usiku wa manane,Amin aliniaga na kuondoka. Usiku huohuo, Amin alimpindua Obote na kuapishwa mnamo mwaka 1967 ili kuwa Rais Kamili. Kilipita kipindi cha juma moja na, mara, nilimuona Amin akiwa dansini na kuahidi kuninunulia vyombo vingi vya muziki kama, yamkini, nitamfundisha kuogelea.
Nilikubali ofa ile kwa shingo upande na, kweli, baada ya mwezi mmoja, aliniletea vyombo vilivyokuwa na uzito wa tani saba! Kwa tukio lile nilitokwa na machozi ya furaha. Lakini, baada ya muda, Amin alianza kuua watu ovyo! Alifika hotelini kwetu, kila jioni, na kuwapiga wazungu kwa kisingizio kuwa alikuwa akiwafundisha weusi! Tuliogopa sana! Taarifa zilizotufikia, kila siku, zilituhakikishia kuwa Amin aliendelea kuua!Hali hii ilinifanya kuhisi kuwa sikuwa salama. Niliamua kutunga uongo na kumuomba msimamizi wa hoteli ili aniruhusu kwenda Misri (Kairo). Nilimwambia kuwa nilitaka kuungana na familia ya Lumumba huko uhamishoni. Hata hivyo, niliporuhusiwa nilielekea Italia.
Nilipofika huko nilianza kupiga muziki wa Waitaliano, shughuli iliyoniingizia pesa.Mnamo mwaka 1973, nilinunua vyombo vya muziki na kuvisafirisha mpaka Uganda. Nilifikia Apollo Hotel na kuanzisha bendi, orginal Makassy na kuhamia sehemu nyingine. Kuhama kwangu hakukuwafurahisha na, kwa sababu hiyo, walihakikisha kuwa muziki wangu haupigwi nchini mwao!
Kuingia Kwangu Tanzania
Tanzania, wakati huo, ilikuwa na bendi moja tu – Maquiz – iliyomilikiwa na Mbombo wa Mbomboka. Mwanamuziki huyu aliniomba ili nije kutumbuiza lakini niliuogopa sana sera ya siasa za Ujamaa na Kujitegemea. Katika falsafa hizi, njia zote za uchumi zilimilikiwa na umma.Mtu yeyote aliyejilimbikizia mali alionekana kuwa adui wa maendeleo, bepari na mnyonyaji!Niliamua kutafuta ushauri kwa waziri mmoja wa Uganda. Yeye alishauri kuwa ingafaa kama ningehamia Kampala, hatua ambayo ingenisaidia kuwakimbia maadui zangu kibiashara. Wapinznani wangu, baada ya kuuona wingi na thamani ya vyombo nilivyoviingiza kutoka Italia, walikosa usingizi! Walitamani sana kuniuua ili, ikiwezekana, waitaifishe mali.
Walianza utekelezaji wa mkakati wao hima. Siku moja, nikiwa Lumumba Night Club, huko Kampala, niliwekwa chini ya ulinzi na Captain Isaya, akinituhumu kuwa sikuwa na stakabadhi ya manunuzi ya vyombo vile. Kwa kuwa niliijua nia yake, nilimwambia kuwa risiti zilisahaulika katika ofisi ya ubalozi huko Kinshasa. Licha ya kushauriwa na kijana mmoja (Mzaire)kuwa nikubaliane nao,sikukubali! Nilikuwa tayari kuuawa. Baada ya kuuona msimamo wangu, afande Maneno alitoa amri niuawe. Mara nilichukuliwa na kupelekwa huko mpakani, Mutukula.
Nikiwa huko, nilikutana na Mkongo mwenzangu aliyetumbuiza kupitia bendi ya kijeshi.Huko tuliswekwa mahabusu na, ilipotimia saa tatu za usiku,tulitupiwa maiti, iliyopigwa na kuvunjwa kichwa, na kutungukia miguuni huku na ikitelekezwa pale kwa siku mbili!
Yule kijana, Mkongo, alikwenda ubalozini (Kampala)na kumtaarifu Gavana (Masullu)kuwa nilishikiliwa na Afande Maneno isivyo halali. Taarifa ile ilimchefua Gavana. Alimpigia simu Isaya na kumtaka anipeleke kwake ama nikiwa hai au nikiwa mfu!Ilipotimu alasiri, Gavana alinipitia ili twende mpirani. Nilifurahi sana kwa kuwa kinyang’anyiro kile kilikuwa kati timu iliyoshabikiwa na gavana na ile niliyoishabikia.Wakati huo, Jeshi waliongoza kwa magoli mawili na kumfanya Gavana kuuliza, kwa furaha, “…Masullu, unaona tunavyowanyanyasa?” Watu waliotuona walionekana kujiuliza nafsini mwao, “… Huyu ni nani aliyeketi na gavana? Mpira ulimalizika kwa timu zote kufungana mabao 2 – 2!
Tukiwa uwanjani,gavana alitaka kujua sababu zilizompelekea Isya kutaka kuniua! Mara, gavana, alitoa bastora na kumtaka Isaya kuhakikisha kuwa ananilinda (mimi Masullu) na kwamba, kama nikipotea, naye ajue kuwa atapotea. Baadaye, tuliongozana na Captain (Gavana) mpaka nyumbani.
Nilivyotelekezwa Porini
Mwaka 1974, nikiwa huko Entebbe, kwenye onesho la muziki mnamo saa 7:00 za usiku, niliwaona askari nilikabiliwa na askari wawili walioniamuru kufunga onesho. Kabla ya kunifikia, walimpiga mtu yeyote alikuwa mbele zao! Walitupandisha kwenye lori lao na kutupeleka umbali wa Kilomita 12.8. Huko waliamuru gari lielekezwe porini. Mateka na askari waliketishwa chini. Tulipofika porini,askari wale walivua sare zao za kijeshi na kuelekea kusikojulikana.Sisi tulitelekezwa huko. Kulipopambazuka tulipobaini kuwa askari wale hawakuwa Waganda, bali lilikuwa kundi la majasusi wa Kiisraeli, waliokuja kuwakomboa ndugu zao walioshikiliwa na Idd Amini! Kutoka huko, tuliokotwa na Wasamaria wema. Wakati huo huo, Balozi wa Zaire, nchini Uganda, aliwasiliana na Station Master, kwa njia ya simu, na kutoa agizo kuwa tupandishwe kwenye treni mpaka Kigoma mjini.
Tulipofika Kigoma, tulikaribishwa kwa shangwe sana! Tulikuta hafla fupi ya harusi kati ya Makongoro Nyererena mkewe. Tafrija hii ilihudumiwa na bendi yetu na, kufuatia kazi nzuri tuliyoifanya pale, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania, Gen. Mayunga, alitusafirisha mpaka Dar es Saalam ili tukatumbuize kwenye kilele cha shamrashamra zile. Tulipangiwa kutumbuiza katika ukumbi wa KMKM, Zanzibar.Tulikubalika sana huko Visiwani. Isivyo bahati,muimbaji mwenzetu, Matingas, alithubutu kuiuza bendi bila ridhaa yetu.Aliutekeleza mpango ule kwa siri sana! Kama asingetokea mtu wa kuniibia siri (kuwa bendi, vyombo na wapigaji wote)walipigwa bei, nisingejua. Kwa kweli, nilichukizwa na hatua ile, hata, nikatishia kujiondoa katika mkataba uliokuwepo. Hata hivyo, niliwahakikishia kuwa nilikuwa radhi kuendelea na kazi ikiwa tu mkataba ule ungepitiwa upya! Nilichukua uamuzi huo kwa sababu bendi yangu ilikuwa miongoni mwa watumbuizaji waliopendwa sana Tanzania.
Mnamo mwaka 1990, nilipokea mwaliko wa kushiriki katika mashindano ya uimbaji wa bendi za muziki huko Mtwara. Waandaaji walinilipa na kuungana ili kutumbuiza huko Mtwara. Lakini tullipofika tu, umeme ulikatika na kupelekea giza nene kutandawaa! Kila walipowasha mishumaa,hawakufanikiwa.Tamasha lililotakiwa kufanyika siku ya Ijumaa halikufanikiwa. Ilipofika Jumamosi,sote tulikubaliana kubadili ukumbi. Pia, shughuli ile ilitakiwa kufanyika katika ukumbi wa Kambarage.Hilo, nalo, halikuwezekana kwa kuwa mvua ilinyesha kuanzia saa 8:00 adhuhuri mpaka saa 1:00 usiku.
Kutoka Mtwara, tulielekea Newala. Huko nako hatukufanikiwa! Safari hii, tuliabiri mpaka Lindi,tukilenga kutumbuiza katika ukumbi wa Officers Mercy, bila mafanikio!Tuliamua kurudi Dar es Salaam. Wenzangu walitumia usafiri wa majini. Mimi nilitumia usafiri wa anga. Nilipoingia tu kwenye ndege, nilihisi kuwa ninaishiwa nguvu. Nilishindwa, hata, kukaa!Wahudumu walinichukua na kunikalisha kwenye kiti na,tangu nilipokaa,sikusogea wala sikujisogeza. Nilipotua katika uwanja wa ndege, marafiki zangu walinipeleka, moja kwa moja, mpaka Kairuki Hospital.Mke wangu aliponiona katika hali ile, alinishauri, “Mume wangu mwambie Yesu.”
Acha Jibu