BOAZ DAVID MWASOTA

  • Mtoto wa Askofu aliyeathirika na dawa za kulevya

“Maisha ya kutumia mihadarati yalinitenga na familia. Jamii yangu ilinichukulia kuwa kama ‘mbwa mwitu,’ aliyeishi katikati ya watu. Niliadahika nikidhani kuwa, kwa kufanya hivyo, ningeondokana na upweke. Kumbe haikuwa hivyo! Nilijiongezea matatizo yaliyochangia kujiangamiza kimaisha. Ashukuriwe Mungu aliyeniona, tokea mbali na kunivuta ili kuniingiza katika pendo lake na kuniondolea aibu.”

Makovu unayoyaona mwilini mwangu yanathibitisha uhalisia wa mateso na manyanyaso niliyopitia nikiwa chini ya utawala wa shetani. Hili laweza kuwa funzo kwa wengine ili wasithubutu kuiga au kuingia kwenye mfumo mbaya wa maisha kama yale.

Nikikumbuka jinsi nilivyowatia aibu wazazi wangu, wanaoendelea kumtumikia Mungu mpaka sasa, hutamani kutubu kila iitwapo leo.

Ninaitwa Boaz David Mwasota, mtoto wa pili kuzaliwa, kati ya watoto watano, katika familia ya Askofu David Mwasota. Nilijipatia elimu ya msingi, darasa la kwanza hadi la tatu, hapa hapa jijini Dar es Salaam, kabla ya kuhamishiwa nchini Uganda ili kuendelea masomo yangu, nikianzia darasa la nne na kuendelea.

  • Nilivyoanza Kutumia Dawa Za Kulevya

Nilianza kutumia mihadarati nikiwa darasa la tano, hali iliyonisababishia upweke kwa kuwa nilikuwa mbali na wazazi wangu. Tabia hii niliambukizwa na Mtanzania, aliyekuwa rafiki yangu (jina linahifadhiwa) na aliyenizidi umri. Nilianza kutumia dawa hizi, kidogo kidogo, huku nikiuamini uongo wake kuwa tabia ile ingeniondolea usongo wa mawazo.

Nilipoanza kutumia dawa za kulevya nilijisikia tofauti sana na nilivyokuwa. Na, kama, Waswahili wasemavyo kuwa “… Safari moja huanzisha nyingine,” nilianza kutumia bangi nikiamini kuwa ingeniondolea mawazo kila nilipowakumbuka wazazi wangu walioishi Tanzania.

Kwa kweli niliwapenda sana wazazi wangu. Niliwakumbuka sana. Kutoka kwenye bangi, niliendelea hadi nikaweza kutumia Heroine. Baada ya muda mrefu, nilishawishika kujiunga na makundi mengine ya vijana wa Kiganda. Wote hawa walikuwa mateja waliopendelea sana muziki aina ya Rege. Niliendelea katika hali hiyo mpaka kufikia kidato cha kwanza na, kwa kuwa nilishindwa kuendelea na masomo, nililazimika kurejeshwa Tanzania.

Wazazi wangu hawakukata tama, waliamua kunipeleka katika shule ya Sekondari ya St. Mary’s ili kuendelea na masomo yangu na kusoma mpaka kidato cha nne huku nikiendelea kutumia bangi. Nailipohitimi elimu ya sekondari (kidato cha nne), na katika kipindi kile ambacho watoto walirejea nyumbani ili kusubiri matokeo ya kujiunga na kidato cha tano na sita, nilikuwa na kawaida ya kwenda uwanjani kuwatafuta wauza unga. Wakati huo nilitumia bangi ambayo gharama yake haikuwa kubwa sana kwangu. Wakati mwingine nilipewa bure tu.

Siku moja niliwakuta marafiki zangu wakitumia aina fulani ya mihadarati ambayo, baada ya kuichunguza, niligundua kuwa ikuwa ni Heroine. Lakini nilipowauliza walinihadaa kuwa wanatumia bange ya daraja la chini. Hivyo nilishawishika hata nikaionja dawa ile na kuhisi hali fulani ya msisimko ambao sikuwahi kuuzoea. Hali ile niliipenda na, ndipo nilipoanza kusaka pesa ili niweze kujipatia mihadarati.

  • Maisha Ya Wizi Yaliyopelekea Kuchukiwa Na Jamii

Kumbuka, niliyafanya haya yote nikiwa mwenda kanisani. Hakuna mtu aliyejua uhalisia wa maisha yangu. Nilijifanya kuwa muombaji huku nikivizia ili kubaini ni wapi mama alipoiweka  pochi yake! Nilikwenda na kuichukua ili,walau, nipate peza za kununulia kete moja ya dawa ya kulevya. Maisha yangu yalighubikwa na matatizo. Kila mmoja alikuwa chonjo alipokuwa karibu nami. Nilipokosa pesa nikaanza kuiba vifaa mbalimbali hapo nyumbani. Nikiona kitu chochote cha thamani ndani nakibeba na kwenda kukiuza kwa bei ya hasara ilimradi tu nipate pesa.

Baadaye nilijikita katika wizi wa vifaa vya ofisi ya baba yangu aliyekuwa Askofu, Kanisani. Niliiba Kompyuta na vito vya thamani. Hukukuwa na kitu kizuri nilichokiacha. Wazazi, pamoja na watu wengine, walinishauri na kunitaka niachane na wizi.

Chupuchupu  Kuchomwa Moto

Hatimaye nilianza safari ya kuwakaba watu, nyakati za usiku, mitaani na, wakati huo huo, nikikata nyavu katika madirisha ya watu. Kuna wakati niliiba pochi ya mama na kukimbilia makundi ya wahuni wenzangu waliokuwa uwanjani. Kila nilipowaza kurudi nyumbani nilihisi kama walikuwa wananiwinda na, kwa sababu hiyo, niliamua kupitia upande wa pili wa ukuta. Nilipojaribu kuruka tu, jirani aliniona na kuniitia ‘mwiziiiii’. Nilipojaribu kuruka, walinikamata na kuanza kunipiga. Walinicharanga mapanga, walinishambulia huku kila mmoja akisema lake.

Wengine walisema kuwa ni heri niuawe kwa kuchomwa moto ati kwa kuwa baba yangu ni Askofu. Walisema kuwa nikipelekwa polisi au gerezani, baba, atatoa pesa na kuachwa huru. Hali hiyo ikiendelea, alitokea baba Asha na, alipotaka kunikata panga, aliambiwa kuwa nilikuwa mtoto wa Mwasota. Aliposikia hivyo, alisita na kuuliza, mtoto wa Mwasota, huyu Askofu ninayemfahamu! Wakamjibu kuwa ndiye! Aliposikia, alishauri nipelekwe polisi. Baadaye walifika marafiki zangu wawili, Amiry na Ali, na kuanza kunitetea. Lakini japo walifanikiwa kuniokoa kwa njia hiyi, watu waliokuwepo hapo walifahamu kuwa tayari niliishapoteza maisha kutokana na kipigo kile. Nilikuwa na hali mbaya. Walipeleka taarifa kwa wazazi wangu kuwa nimefariki dunia. Walipofika hapo Polisi walinichukua hadi hospitali moja ya binafsi kwa matibabu.

Nashukuru Mungu, nilipata msaada wa haraka wa madakatari, japo hali yangu ilikuwa mbaya. Nilitibiwa hospitalini hapo kwa miezi kadhaa na badaye nilipopata nafuu, walishauri kuwa nihudhurie dawati la watu walioathirika na dawa za kukevya(Soberer), ili nipate msaada.

  • MUUJIZA WANGU WA KWANZA    

Nakumbuka nikiwa hapo walimuita mama yangu na kumueleza utaratibu wa kusaidia watu kama mimi ikiwa ni sambamba na kupewa dawa kidogo kidogo hadi nitakapofikia hatua ya kutoka katika hali hiyo.  Kwangu mimi nashukuru haikutokea hivyo kwani nilihisi kupoteza hamu, pia nilijua mama yangu asingekubaliana na hilo kwakuwa alikuwa mtu wa Mungu asiyeamini uponyaji kwa njia hiyo. Nilimueleza mama kuwa mimi sintotumia tena dawa hizo, japo nilikuwa bafdo navuta sigara. Nakumbuka nilianza kuhisi badiliko fulani ndani yangu. Nikahisi kuanza kumsifu Mungu na kuimba nyimbo za kumuinua .

Nikiwa katika hali hiyo nilirejea nyumbani na kuomba kwenda kanisani, japo watu bado walikuwa na shaka nami wakikumbuka na  wakirejelea maisha yangu ya awali. Kuanzia hapo nilianza kubadilika na kuwa mtu mwema nikaanza kujiunga na makundi ya maombi kanisani. Nikiachana na makundi yasiyofaa.  Nikampa Yesu maisha yangu na kuendelea na maisha ya wokovu. Tokea hapo Yesu akaanza kunifinyanga upya.  Ninapokumbuka vijana wenzangu waliopoteza maisha na wengine niliowaacha mitaani inaniuma sana. Na hii ndiyo iliyonisukuma kuanzisha shirika la ‘BE WISE’ inayoshughulika na elimu kwa makundi rika, waachane na uvutaji wa dawa za kulevya.

Nashukuru Mungu kwa kunitetea hadi kuniondoa katika mateso hayo. Ninachoamini ni kwamba, huwezi kuondoka katika kifungo cha aina hii bila msaada wa Yesu. Nikushauri kijana mwenzangu,  unayepita katika hali kama hiyo, kumkimblilia Yesu, kwani yeye anaweza kubadilisha maisha yako. Mungu ameniwezesha na sasa nimeoa na mtoto  mmoja. Sasa naishi maisha ya amani na furaha tele ndani ya Yesu.

Kushiriki ni kujali!

Acha Jibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *